Mkurugenzi Mtendaji wa Devan Communication Consultancy na Mwandaaji wa Tamasha la Wadau wa Chakula Tanzania, Salima Mseta akizungumza kwenye Tamasha la Mashefu Tanzania lililofanyika mkoani Arusha

Mkurugenzi Mtendaji wa Devan Communication Consultancy na Mwandaaji wa Tamasha la Wadau wa Chakula Tanzania, Salima Mseta akizungumza kwenye Tamasha la Mashefu Tanzania lililofanyika mkoani Arusha

Na Happy Lazaro, Arusha
Mashefu na wadau wa sekta ya chakula nchini wametakiwa kutumia fursa zinazojitokeza katika sekta hiyo kwa kuunganisha nguvu na kuendeleza vyakula vya asili ili viweze kutambulika na kupata masoko zaidi ndani na nje ya Tanzania.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa Devan Communication Consultancy na Mwandaaji wa Tamasha la Wadau wa Chakula Tanzania, Salima Mseta wakati akizungumza kwenye Tamasha la Mashefu Tanzania lililofanyika mkoani Arusha .
Salima amesema tamasha hilo lililowakutanisha mashefu na wadau mbalimbali wa sekta ya chakula lengo ni kubadilishana uzoefu, kuonesha ubunifu wa mapishi na kujadili fursa zilizopo katika sekta hiyo.
Amesema wadau wanaojihusisha na vyakula vya asili, pamoja na wanaozalisha na kuuza vyakula, wanapaswa kuunganisha nguvu na kuanzisha miradi itakayosaidia kuendeleza bidhaa hizo na kuzifanya ziwe na thamani zaidi katika soko.
Salima amesema chakula ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Tanzania na kina nafasi kubwa katika kukuza utalii, huku akisisitiza umuhimu wa maandalizi kuelekea AFCON 2027.
“Tanzania inapaswa kutumia fursa ya AFCON 2027 kutangaza utamaduni wake, ikiwemo vyakula vya asili, kwa wageni watakaofika nchini kutoka mataifa mbalimbali.”amesema Salima .
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wapishi, hoteli, migahawa na wadau wengine wa sekta ya chakula katika kuhakikisha Tanzania inajiandaa vyema na kutumia fursa zinazotokana na matukio makubwa ya kimataifa.
“Vyakula vya asili kama kitumbua, magimbi, mchemsho na vyakula vingine vinaweza kuendelezwa na kutambulishwa kwa ubora unaokubalika, badala ya kuviangalia kama vyakula vya kawaida visivyo na fursa kubwa ya kibiashara.”amesema Salima .
Ameeleza kuwa ni muhimu pia wadau kuzingatia taratibu za kisheria, ikiwemo kupata leseni na vibali vinavyohitajika, ili biashara za vyakula vya asili ziweze kukua na kufikia masoko rasmi.
“Watu wa vyakula vya asili na watu ambao wanazalisha vyakula na kuuza, wote tuweke miradi ya kufanya chakula kile cha asili kionekane na kipate soko,” amesema Salima .
Ameongeza kuwa , juhudi hizo zinaweza kusaidia kuitangaza Tanzania kupitia vyakula vyake vya asili na viungo, huku zikitoa nafasi kwa wajasiriamali na wazalishaji kuongeza kipato kupitia biashara ya chakula.
Ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia wizara na taasisi mbalimbali imeendelea kutambua umuhimu wa sekta ya chakula, hivyo wadau wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuwekeza na kuibua ubunifu unaoweza kuleta matokeo ya kiuchumi.
“Tamasha hilo limekuwa pia fursa kwa mashefu kuonesha umahiri wao katika mapishi na kujifunza mbinu mbalimbali za kuboresha maandalizi, uwasilishaji na ubora wa vyakula ili kukidhi mahitaji ya soko la kisasa.”amesema Salima .
Ameongeza kuwa,tamasha hilo limeweka msisitizo katika umuhimu wa kuunganisha sekta ya chakula na maeneo mengine kama utalii na biashara, kwa kuwa vyakula ni sehemu muhimu ya utambulisho wa utamaduni na kivutio kwa wageni wanaotembelea Tanzania.
Tamasha la Mashefu Tanzania limeendelea kutoa jukwaa la kukutanisha wadau wa sekta ya chakula, huku washiriki wakihimizwa kuchangamkia fursa zilizopo, kuendeleza vyakula vya asili na kushirikiana katika kujenga sekta yenye tija kwa uchumi na jamii.
Kwa upande wake mgeni rasmi wa Tamasha hilo, , Rais wa Africa Chefs Alliance, Chief Shaun Smith,
amesema mpishi anahitaji kuwa na mpangilio mzuri wa kazi, kuzingatia usalama wa chakula, kushirikiana na wadau wengine pamoja na kupunguza upotevu wa chakula.
Chief Shaun amesema ushirikiano miongoni mwa wapishi na wadau wa sekta ya chakula ni muhimu katika kuimarisha sekta ya upishi na utalii barani Afrika, huku akisisitiza kauli ya “One Africa – Une Afrique.”
Tamasha la Tanzania Chefs Culinary Festival limeendelea kuwa jukwaa la kuwaunganisha wapishi na wadau wa chakula, kukuza vipaji na kuhamasisha matumizi na utangazaji wa vyakula vya asili vya Tanzania.
