Serikali imewataka Makandarasi wanawake kutumia miradi wanayopewa kutekeleza kama fursa ya kuonesha uwezo wao, kujenga uaminifu na kujipatia nafasi ya kutekeleza miradi mikubwa na mingi zaidi nchini.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, wakati akifungua Kongamano la Sita la Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania (TWCA), lililofanyika jijini Dar es Salaam chini ya kaulimbiu isemayo “Wezesha, Jenga, Stawi.”
Waziri Kadogosa amesema kuwa makandarasi wanawake wanapaswa kujituma na kuhakikisha wanatekeleza miradi wanayopewa na Serikali kwa kuzingatia ubora, weledi na viwango vinavyotakiwa ili kujenga imani kwa wateja na kupata fursa zaidi za kazi.
“Hakikisheni kazi ndogo mnazozipata mnazitumia kama fursa ya kupata kazi zaidi. Onesheni uwezo wenu. Taifa linahitaji wanawake wenye uwezo wanaopewa nafasi na kutekeleza kazi kama inavyotakiwa,” amesema Kadogosa.
Aidha, Waziri Kadogosa ameeleza kuwa Serikali, kupitia Sekta ya Ujenzi, inalenga kuona wanawake wakishiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa kuwa waajiri, makandarasi, wamiliki wa kampuni, wataalamu na wabunifu katika sekta hiyo.
Halikadhalika, amewapongeza makandarasi hao kwa jitihada zao katika utekelezaji wa miradi mikubwa, ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya lami mkoani Songwe ulioshirikisha kampuni zaidi ya 15.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa jitihada mnazofanya katika kutekeleza miradi. Kupitia jitihada hizo, Serikali imechukua hatua ya kuongeza malipo ya awali kutoka asilimia 15 hadi asilimia 30,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, amesema Wizara hiyo, kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), itaendelea kukiunga mkono chama hicho na kuhakikisha makandarasi wanawake wanapata fursa mbalimbali za kuwawezesha kukua kitaaluma na kibiashara, ikiwemo mafunzo ya kuwajengea uwezo.
Naye, Rais wa TWCA, Bi. Judith Odunga, ameishukuru Serikali kwa kukipa kipaumbele chama hicho na kuwezesha makandarasi wanawake kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya barabara yenye urefu wa kilomita 20 mkoani Songwe, pamoja na kuwapatia mafunzo ya usimamizi wa fedha na miradi.
Kongamano hilo la Sita limewakutanisha makandarasi wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya sekta hiyo na mustakabali wa ushiriki wa wanawake katika shughuli za ujenzi.

