Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Udhamini wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), Mwanahiba Mzee, amesema mfuko huo umetenga Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kutoa dhamana ya mikopo kwa vijana na wanawake kupitia Benki ya Azania, hatua inayotarajiwa kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye thamani ya kati ya Shilingi bilioni 20 hadi bilioni 80, kutegemeana na kiwango cha dhamana kitakachotumika.

Ameyasema hayo Oktoba 09,2026 wakati wa hafla ya kusaini ushirikiano kati ya AGITF na Benki ya Azania, akibainisha kuwa dhamana ya mfuko huo inaweza kufikia asilimia 50 ya mkopo, ili kuwawezesha vijana na wanawake wasiokuwa na dhamana za kutosha kupata mikopo kwa masharti nafuu. Aidha, amesema fedha hizo zitatolewa baada ya kukamilika kwa taratibu za nyaraka na kuidhinishwa na bodi. Amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha utekelezaji wa programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), iliyoanzishwa na Wizara ya Kilimo mwaka wa fedha 2022/2023, kwa kuwezesha mitaji kwa vijana na wanawake wanaojihusisha na shughuli mbalimbali za kilimo, ikiwemo uzalishaji wa mazao, ufugaji na uvuvi.

Amebainisha kuwa kupitia ushirikiano huo, AGITF na Benki ya Azania pia zitashirikiana katika kutoa elimu ya kilimo na usimamizi wa fedha, kujenga uwezo wa vijana na wanawake, pamoja na kuboresha mifumo ya urejeshaji wa mikopo. Amesema elimu hiyo ni muhimu ili kuwasaidia wakulima kutambua gharama halisi za uzalishaji na faida wanazopata katika shughuli zao.

Aidha, amesema AGITF haijaacha kabisa kutoa mikopo moja kwa moja kwa wanufaika, bali inaendelea na utaratibu huo kwa kiwango kidogo pale taasisi za fedha zinaposhindwa kuwafikia baadhi ya vijana na wanawake. Ameeleza kuwa lengo ni kuendelea kutoa dhamana na fedha kupitia taasisi za fedha ili mikopo ipatikane kwa masharti himilivu na kufikia wanufaika wengi zaidi.

Akizungumzia wigo wa programu ya BBT, Mwanahiba amebainisha kuwa programu hiyo haijahusishwa na vijana walioko kwenye kambi za Chinangali na Ndugai pekee, bali inalenga vijana na wanawake wote Tanzania Bara. Amesema tangu kuanza kwa programu hiyo, mikopo imewafikia wanufaika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Njombe, Kagera, Tabora, Arusha, Singida na Dodoma.Amesema ushirikiano huo unatarajiwa pia kufungua fursa za uwekezaji katika miradi ya kilimo inayohitaji mikopo ya muda mrefu, ikiwemo kilimo cha parachichi na kahawa, ambayo inahitaji muda kabla ya kuanza kutoa mavuno. Ameongeza kuwa mafanikio ya ushirikiano huo yatapimwa kwa ongezeko la ajira, uzalishaji, tija na kipato cha wakulima.Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Biashara za Kilimo na SMEs wa Benki ya Azania, Augustino Matutu, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dkt. Esther Mang’enya, amesema benki hiyo imetoa mikopo ya zaidi ya Shilingi bilioni 700 katika sekta ya kilimo kwa miaka mitano iliyopita. Amebainisha kuwa ushirikiano na AGITF utawawezesha vijana na wanawake kupata mikopo yenye masharti nafuu, wakiwemo wasiokuwa na dhamana za kutosha.

Matutu amesema benki hiyo inatumia mikopo ya vikundi kuwafikia wakulima wadogo vijijini, huku ikizingatia uzoefu, rekodi za uzalishaji na upatikanaji wa masoko kabla ya kutoa mikopo.

Aidha, amesisitiza kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza tija na kupunguza utegemezi wa mvua. Amesema benki hiyo inatoa mikopo ya kuchimba visima vya umwagiliaji inayoweza kurejeshwa ndani ya miaka mitatu hadi mitano.