* Prof. Shemdoe awapongeza walimu wa Geita kwa mafanikio katika sekta ya elimu
* Dkt. Biteko asisitiza uwekezaji katika elimu na kuthamini mchango wa walimu. 
* Serikali imelipa madeni ya watumishi mkoani Geita
* Dkt. Biteko ampongeza Rais Samia kwa kuendeleza sekta ya elimu
Bukombe, Geita
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewapongeza walimu wa Mkoa wa Geita kwa mafanikio katika sekta ya elimu, huku akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na weledi ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Prof. Shemdoe ametoa pongezi hizo leo, Oktoba 9, 2026, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yaliyofanyika wilayani Bukombe, mkoani Geita, yaliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko, kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa walimu katika maendeleo ya elimu.
Amesema Mkoa wa Geita umeendelea kufanya vizuri katika sekta ya elimu kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa na ya tisa kitaifa katika ufaulu, mafanikio aliyoyahusisha na juhudi za walimu pamoja na ushirikiano wa wadau wa elimu.
Aidha, Prof. Shemdoe amempongeza Dkt. Biteko kwa kuandaa maadhimisho hayo yaliyowakutanisha walimu wa Bukombe, kuwapa fursa ya kusherehekea siku yao, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika elimu na kuthamini mchango wa walimu, akisema mwalimu ndiye msingi wa maarifa na maendeleo ya jamii.
“Mwalimu humpa mtoto maarifa,” amesema Dkt. Biteko, akieleza kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuwapa walimu fursa ya kufurahia siku yao na kutambua kazi kubwa wanayoifanya katika kujenga taifa lenye maarifa na ujuzi.
Dkt. Biteko pia amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya elimu kupitia uwekezaji katika miundombinu, kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na maslahi ya walimu.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Mohamed Gombati, amesema Serikali imeendelea kuboresha maslahi na kuwajengea uwezo watumishi, ikiwemo kulipa madeni ya watumishi yenye thamani ya shilingi bilioni 8, hatua inayolenga kuongeza ari na ufanisi katika utendaji kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Muragili, amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya elimu wilayani humo, huku akipongeza juhudi za Dkt. Biteko katika kusimamia na kuhamasisha maendeleo ya sekta hiyo, ambazo zimechangia kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi.
Naye Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Bukombe, Bi. Jenipher Kisusi, amesema maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka tangu 2019, yakilenga kuthamini mchango wa walimu, kuimarisha mshikamano na kutoa tuzo kwa shule zinazofanya vizuri kitaaluma.
Kwa upande wao, walimu wa Bukombe wameishukuru Serikali na viongozi kwa kutambua mchango wao, huku wakiahidi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi na uzalendo ili kuinua kiwango cha elimu wilayani humo.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa wito kwa walimu, wazazi, viongozi na wadau wa elimu kuendelea kushirikiana katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kudumisha maadili, ili kuhakikisha elimu bora inakuwa msingi imara wa maendeleo endelevu ya Bukombe na Taifa kwa ujumla.
