Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, ametembelea Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) jijini Dodoma, ambapo amejionea namna Mamlaka hiyo ilivyojipanga katika kuhakikisha wateja na wadau wa sekta ya ununuzi wa umma wanapata huduma bora, zenye viwango na zinazokidhi mahitaji yao.

Katika ziara hiyo iliyofanyika jana Oktoba 8, 2026, Bi. Senyamule alitembelea maeneo mbalimbali yanayotumika kutoa huduma kwa wateja, yakiwemo eneo la mapokezi, Chumba Maalum cha Msaada wa Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST), pamoja na Ofisi za Kituo cha Huduma za Msaada wa Kitaalamu kwa Wateja (Call Centre).

Akiwa katika maeneo hayo, Mkuu wa Mkoa alielezwa namna mifumo na vitengo hivyo vinavyoratibu upokeaji wa wateja, kutoa maelekezo, kujibu maswali na kuwasaidia watumiaji wa mfumo wa NeST wanapokutana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma.

Bi. Senyamule alionesha kufurahishwa na namna PPRA ilivyojipanga katika kuweka mazingira rafiki kwa wateja, kuimarisha upatikanaji wa huduma na kuhakikisha kuwa wateja wanapata msaada unaohitajika kwa wakati. Ziara hiyo pia ilimpa fursa ya kufahamu juhudi zinazofanywa na Mamlaka katika kurahisisha mawasiliano na wateja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, alieleza kuwa Mamlaka inawatambua na kuwathamini wateja wake kama sehemu muhimu ya utekelezaji wa majukumu yake. Alisisitiza kuwa PPRA imejipanga kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wateja na wadau wanapata huduma bora, kwa kuzingatia mahitaji yao na viwango vinavyotarajiwa katika utoaji wa huduma kwa umma.

Alieleza kuwa thamani ya mteja ni nguzo muhimu katika utendaji kazi wa PPRA, hivyo Mamlaka inaendelea kuimarisha mifumo na njia mbalimbali za utoaji wa huduma ili kuhakikisha wateja wanahudumiwa kwa ufanisi, wanapata ufafanuzi wa masuala yanayowakabili na kusaidiwa kutatua changamoto zinazohusiana na mifumo na taratibu za ununuzi wa umma.

Bw. Simba aliongeza kuwa kuwepo kwa eneo maalum la mapokezi, chumba cha msaada wa mfumo wa NeST na kituo cha Call Centre ni sehemu ya jitihada za PPRA za kuboresha uzoefu wa wateja na kuhakikisha kuwa huduma zinapatikana kupitia njia zinazowawezesha kupata msaada unaohitajika. Huku akitoa wito kwa Wananchi kuendelea kufika ofisi sita za kanda ikiwemo kanda ya Pwani yenye ofisi zake Jijini Dar es Salaam, kanda ya Kaskazini yenye Ofisi Jijini Arusha, Kanda ya Kati na Magharibi, Yenye Ofisi Mkoani Tabora, Kanda ya Ziwa yenye Ofisi Jijini Mwanza, kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye ofisi Jijini Mbeya na Kanda ya Kusini yenye ofisi Mkoani Mtwara. 

Ziara hiyo imetoa taswira juu ya dhamira ya PPRA ya kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja na wadau wa sekta ya ununuzi wa umma, kwa kuweka kipaumbele katika mahitaji yao, kuboresha mawasiliano na kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa katika Makao Makuu na ofisi za kanda za Mamlaka hiyo.

PPRA inaendelea kuwahimiza wateja na wadau wote kutembelea ofisi zake na kutumia njia rasmi za mawasiliano zilizowekwa ili kupata elimu, maelekezo na msaada wa kitaalamu kuhusu masuala mbalimbali kuhusu tenda za serikali na ununuzi wa umma kwa ujumla.