Wakati maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa yakiwa katika siku ya pili, leo tarehe 9 Oktoba 2026, banda la VETA limekuwa na mvuto wa kipekee likikusanya wadau na wananchi kwa ujumla kushuhudia umahiri wa vijana wahitimu wa ufundi stadi, hususani wenye ulemavu kutoka vyuo mbalimbali vya VETA.
Katika maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi, Nduwa chini ya kaulimbiu, _Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana_, VETA inawakilishwa na vijana wahitimu na wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya VETA, wengi wao wakiwa ni wenye ulemavu, hivyo kutafsiri kaulimbiu hiyo kwa vitendo zaidi.
Miongoni mwa wahitimu hao ambao wameonesha umahiri mkubwa na kuwa kivutio kikubwa cha wadau na wananchi katika maonesho hayo ni pamoja na wanafunzi wenye ulemavu wa viungo Francis Madanganya, mhitimu wa stadi ya TEHAMA kutoka Chuo cha TEHAMA cha VETA Kipawa na Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro ambaye ana ubunifu wa Power Bank ya kompyuta mpakato (laptop); Gonsalva Lungu mhitimu wa Stadi ya Ubunifu, Ushonaji na Teknolojia ya Nguo kutoka chuo cha VETA Songea; Riziki Ndumba, mhitimu wa Stadi ya Ubunifu, Ushonaji na Teknolojia ya Nguo kutoka chuo cha VETA Songea; Imelda Kanyengele, mwanafunzi wa Ngazi ya Pili stadi ya Ubunifu, Ushonaji na Teknolojia ya Nguo, Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Nkasi na Ernest Mashiku Igobeko, mhitimu wa stadi ya Useremala kutoka Chuo cha VETA Tanga, ambaye ana ulemavu wa uoni (asiyeona).
Miongoni mwa wadau walioonesha kuvutiwa zaidi na wahitimu na wanafunzi hao ni kutoka Benki ya CRDB ambao wamewaunga mkopo papo kwa papo kwa kununua bidhaa zao na kuwachangia fedha kwa ajili ya kukuza mitaji ya shughuli zao.
Meneja wa Mahusiano na Taasisi za Serikali wa Benki ya CRDB, Paskalina Diu, amesema wataangalia namna ya kuwawezesha vijana hao kunufaika na fursa za mikopo na huduma za kifedha zitakazowasaidia kuendeleza shughuli.
Amesema benki hiyo ina vitengo mbalimbali vinavyolenga kuwawezesha vijana kiuchumi, ikiwamo CRDB Bank Foundation, inayotoa mitaji wezeshi isiyo na riba.
“Kupitia kliniki ya CRDB Bank Foundation, tutaangalia namna bora ya kuwasaidia vijana wanaopata mafunzo ya ufundi stadi ili watumie ujuzi wao kujiajiri na kukuza shughuli zao za kiuchumi,” amesema.
Katika hatua nyingine, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa fani ya ushonaji katika Chuo cha VETA Nkasi, Imelda Kanyengele, amesema mafunzo anayopata yamemwezesha kushona aina mbalimbali za nguo na kutengeneza batiki.
“Katika chuo chetu nimejifunza mambo mengi, yakiwamo ushonaji wa nguo za aina mbalimbali pamoja na utengenezaji wa batiki. Nilikuwa sitarajii kama ningefikia kiwango hiki, lakini kwa sasa ninaweza kushona aina mbalimbali za nguo,” amesema Imelda.
Amewahimiza vijana wenzake, hususan wenye ulemavu, kutokata tamaa katika kutafuta elimu na ujuzi utakaowawezesha kujitegemea.
Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yalianza jana tarehe 8 Oktoba, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa Tarehe 14 Oktoba, 2026, mjini Sumbawanga na yanatarajiwa kufunguliwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
