Na WMMJWM Dar Es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa masuala ya jinsia wameweka mikakati ya utekelezaji wa vipaumbele vya kitaifa vya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kupitia miradi na programu mbalimbali.Hatua hiyo imefikiwa leo Oktoba 09, 2026 mkoani Dar Es Salaam katika kikao kilicholenga kubadilishana taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi na programu na za masuala ya jinsia, pamoja na kuainisha maeneo ya ushirikiano na fursa za kuimarisha mchango wa wadau wa maendeleo katika kufikia vipaumbele vya kitaifa.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Eliakim Chacha Maswi amesema katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050), utekelezaji wa miradi na programu zinazolenga masuala ya jinsia ni muhimu kuzingatia wanawake wanapata fursa sawa katika masuala ya kiuchumi, huku msisitizo ukiwekwa katika utekelezaji wake kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau.

Ameongeza kuwa katika kutekeleza hayo Wizara imeandaa Ajenda ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kijamii na Maendeleo ya Mtaji Watu katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Jamii Ajenda – Dira 2050) ili kufanikisha utekelezaji wa Dira 2050 ili kuimarisha familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Zanzibar, Abeida Rashid Abdallah amesema Wizara hiyo imekuwa ikishirikiana na wadau hao katika kutekeleza miradi na programu zinazolenga kuwekeza katika usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi katika maeneo mbalimbali huko Zanzibar.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wadau hao Miranda Amstrong kutoka Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha miradi na programu za masuala ya jinsia inatekelezeka kwa kutoa mchango wao wa rasilimali fedha na kuwajengea uwezo wasimamizi na watekelezaji wa miradi na programu hizo.