Na. Meleka Kulwa– Fullshangwe Blog, Dodoma

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Prof. Abel Makubi ,amewataka Madaktari kuimarisha uchunguzi wa mapema wa upungufu wa damu na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa wakati ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza, hususan kwa wajawazito na watoto. 

Akizungumza Oktoba 9, 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kliniki mbili za upungufu wa damu na tatizo la moyo wa wajawazito na watoto amesema kuwa umuhimu wa kufuatilia afya za wagonjwa na kuchunguza mabadiliko yanayoweza kuashiria uwepo wa tatizo hilo hivyo ni muhimu kujua afya ya mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua.

Amesema wataalamu wa afya wanapaswa kuzingatia mabadiliko ya kiwango cha hemoglobini katika damu ya mgonjwa na kuchunguza chanzo chake badala ya kusubiri hali izidi kuwa mbaya kwa kiwango hicho hatua kwa hatua kunahitaji ufuatiliaji wa kitaalamu ili kusaidia kubaini tatizo mapema na kupanga matibabu yanayofaa.“upungufu wa damu ni changamoto inayopaswa kupewa kipaumbele wajawazito na watoto ni miongoni mwa makundi yanayohitaji uangalizi wa karibu ivyo basi umuhimu wa kupima afya na kutafuta huduma za kitabibu kwa wakati ni sehemu muhimu ya kukabiliana na tatizo hilo,” amesema Prof. Makubi

Katika kuimarisha huduma za kibingwa, Hospitali ya Benjamin Mkapa imezindua kliniki mbili mpya, ikiwemo kliniki maalumu ya upungufu wa damu na kliniki jumuishi inayohusisha huduma za magonjwa ya moyo na wajawazito. Hatua hiyo imeongeza idadi ya kliniki za hospitali hiyo kutoka 24 hadi 26 ikiiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua huduma na kukidhi mahitaji ya wagonjwa.

Akisisitiza umuhimu wa huduma bora kwa wagonjwa Prof. Makubi ameeleza kuwa uchunguzi wa mapema na ufuatiliaji wa matibabu na utoaji wa elimu ya afya kwa jamii ni hatua muhimu zinazoweza kusaidia kupunguza madhara ya magonjwa. Amehimiza wananchi kutopuuzia mabadiliko ya afya zao na kufika hospitalini wanapohitaji uchunguzi au ushauri wa kitaalamu.Kwa Upande wake Beatrice Faustine, mkazi wa Mnada Mpya jijini Dodoma ambaye  mtoto wake alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ameishukuru hospitali hiyo kwa huduma alizopata kutoka kwa madaktari amesema alipokelewa vizuri, mtoto wake akafanyiwa vipimo na kuandikiwa dawa, huku akieleza kuwa hali ya mtoto ilianza kuimarika baada ya kuanza matibabu.

Amesema hali ya mtoto wake imeendelea kuimarika baada ya kuanza matibabu, huku akieleza kuwa anaendelea kufuata maelekezo ya madaktari na kurejea hospitalini kwa ufuatiliaji na baada ya siku mbili za matibabu, mtoto wake alianza kutembea vizuri, jambo lililompa matumaini kuhusu maendeleo ya afya yake.

“Nimeambiwa mtoto wangu anaendelea vizuri na nitaendelea kutumia dawa nilizopewa. Nimepewa dawa za mwezi mmoja, na mwezi utakapoisha nitarudi tena hospitalini.”amesema Bi. Faustine.

Kuanzishwa kwa kliniki hizo mpya katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kunatarajiwa kusaidia kupanua upatikanaji wa huduma za kibingwa. Pamoja na hatua hiyo, elimu kwa jamii, uchunguzi wa mapema na ufuatiliaji wa matibabu vinaendelea kuwa mambo muhimu katika kuboresha afya za wananchi, hasa wajawazito na watoto wanaohitaji uangalizi maalumu.