Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya St. Mary’s Duluti, Matei Malya,akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arusha

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Mary’s Duluti, Bro. Protas Mangu akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha 

………..

Na Happy Lazaro, Arusha

Serikali imetakiwa kuendelea kuboresha mitaala ya elimu na kusimamia utekelezaji wake, hususan katika masomo ya Amali, ili kuwawezesha wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne, kidato cha sita na vyuo vya kati kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri badala ya kutegemea ajira kutoka serikalini.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya St. Mary’s Duluti, Matei Malya, wakati wa mahafali ya 17 ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo mkoani Arusha, akisisitiza umuhimu wa elimu inayomwandaa mwanafunzi kutumia maarifa aliyoyapata kujenga maisha yake na kuchangia maendeleo ya jamii.

Malya amesema kuwa serikali, wazazi, walezi na wadau wa elimu wanapaswa kuongeza juhudi katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu yenye maarifa na ujuzi wa vitendo utakaowasaidia kujitegemea baada ya kuhitimu masomo katika ngazi mbalimbali.

Amesema maboresho ya mitaala yanapaswa kwenda sambamba na usimamizi madhubuti wa utekelezaji wake ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kubuni fursa za kiuchumi katika fani mbalimbali, badala ya kuhitimu wakiwa na matarajio pekee ya kuajiriwa.

Ameeleza kuwa ubunifu uliooneshwa na wanafunzi katika shughuli mbalimbali ni ushahidi kuwa elimu inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kujenga ujasiriamali, iwapo watapatiwa maarifa na ujuzi unaolingana na mahitaji ya jamii na soko la ajira.

“Hapa tayari kila mmoja wetu ameona namna ambavyo hawa watoto walivyo wabunifu na wanaenda kujiajiri. Hivyo, tukiboresha mitaala, watu hawatalia ajira sana bali watajiajiri,” amesema Malya.

Aidha, amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha watoto wanapata mahitaji muhimu ya shule, yakiwemo sare, karo, ada na vitabu, huku wakifuatilia kwa karibu maendeleo yao ya kitaaluma na kitabia wanapokuwa shuleni.

Malya amesema ushirikiano kati ya wazazi, walimu na serikali ni muhimu katika kujenga mazingira bora ya kujifunzia na kuwaandaa wanafunzi kuwa watu wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha baada ya kumaliza elimu ya sekondari.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Mary’s Duluti, Bro. Protas Mangu, amewataka wahitimu kuendelea kuzingatia maadili mema waliyojifunza shuleni hapo na kuyaishi katika jamii zinazowazunguka ili waweze kufikia malengo yao ya baadaye.

“Shule yetu tumekuwa tukiwaandaa watoto kuweza kujiajiri kwa kuwafundisha masomo kwa vitendo kama mlivyojionea hapa jinsi ambavyo wana ubunifu mkubwa katika kutengeneza vitu mbalimbali na lengo letu wakitoka hapa wakaweze kujiajiri wenyewe popote watakapokuwa.”amesema Bro.Mangu.

Bro.Mangu amewahimiza wahitimu kumtanguliza Mungu katika maisha yao, kuwa na nidhamu na kujiamini katika kutekeleza majukumu yao, akieleza kuwa misingi hiyo itawasaidia kufanya maamuzi sahihi na kuwa raia wenye mchango chanya katika jamii.

“Nawaomba sana mtangulize Mungu na muweke nidhamu ya maisha katika kufikia malengo yenu, na muwe na ujasiri wa kujiamini na kutenda kila jambo jema katika jamii inayowazunguka,” amesema Bro Mangu.

Ameongeza kuwa wahitimu wanapaswa kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu maisha yao ya baadaye, ikiwemo ulevi, uvivu na kujihusisha na matumizi yasiyofaa ya mitandao ya kijamii, badala yake wajenge tabia ya uwajibikaji, usikivu na kuishi kwa uadilifu.

Bro.Mangu amewataka pia kuepuka tamaa ya kutafuta mafanikio kwa njia zisizo halali, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, kuwa na subira na kuzingatia misingi ya maadili katika kutimiza ndoto zao.

Naye Padre Adolf Msoka amewataka wahitimu kuendelea kulishika na kulitekeleza neno la Mungu popote watakapokuwa, huku wakidumisha maadili na kuendeleza maarifa pamoja na misingi mema waliyojengewa wakati wa masomo yao shuleni hapo