Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo , ambaye ni Mbunge wa Arusha mjini ,Paul Makonda akizungumza na wananchi kwenye ziara hiyo jijini Arusha
Mwakilishi wa Mkandarasi kutoka kampuni ya CCECCanayetekeleza mradi wa barabara ya Mbauda , Mhandisi Huang Yufeng akizungumzia kuhusu mradi huo jijini Arusha.
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo , ambaye ni Mbunge wa Arusha mjini ,Paul Makonda amesema wananchi wanaendelea kuwa na imani na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara unaolenga kuboresha usafiri na kuunganisha maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza na wananchi katika ziara ya Waziri wa ujenzi Masanja Kadogosa alipotembelea barabara mbalimbali zinazoendelea kujengwa mkoani Arusha .
Makonda amesema wananchi wa maeneo yanayopitiwa na mradi huo wamekuwa wakishuhudia matokeo ya utekelezaji wa ahadi za Serikali, jambo ambalo limeendelea kuimarisha imani yao kwa Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha Makonda ameishukuru Wizara ya Ujenzi kwa ushirikiano uliotolewa katika kufanikisha miradi ya barabara Arusha, akiwapongeza viongozi na wataalamu wa wizara, wakiwemo Katibu Mkuu na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, kwa kusikiliza mahitaji ya wananchi na kuyafanyia kazi.
Waziri Makonda, amesema matarajio yake ni kuona mradi huo unakamilika kwa wakati, ukiambatana na ujenzi wa taa za barabarani, vituo vya mabasi pamoja na upandaji wa miti kwa lengo la kulipendezesha zaidi jiji la Arusha.
Makonda ameomba ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 1.9 kutoka Roundabout ya Kisongo hadi Matevesi kupewa kipaumbele, akieleza kuwa ujenzi huo utasaidia kufungua zaidi jiji la Arusha kwa miundombinu na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.
Amesema anaamini chini ya kasi ya uongozi wa Waziri wa Ujenzi, miradi ya barabara inayoendelea Arusha itakamilishwa kwa wakati na kuwawezesha wananchi kutumia miundombinu ya lami kama ilivyoahidiwa na Serikali.
“Utekelezaji wa ahadi za Serikali ni muhimu katika kujenga imani ya wananchi, kwani wananchi wa Arusha kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya barabara mbovu katika maeneo mbalimbali.”amesema Waziri Makonda .
Amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha miundombinu hiyo zimeanza kuleta matumaini mapya kwa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi hiyo inakamilika na kuanza kutumika kwa manufaa ya wananchi.
Ameishukuru Serikali nzima kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya Arusha, akisema barabara hizo zitakapokamilika zitasaidia kurahisisha usafiri, shughuli za kiuchumi na kuunganisha maeneo mbalimbali ya jiji.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkandarasi kutoka kampuni ya CCECCanayetekeleza mradi wa barabara ya Mbauda , Mhandisi Huang Yufeng, amesema ujenzi wa barabara kutoka mbauda hadi mzunguko wa CCM wenye urefu wa kilomita 7.4 unaendelea vizuri, huku mradi huo ukifikia asilimia 52 ya utekelezaji tangu kuanza kwa kazi mwezi Mei mwaka huu.
Amesema lengo la mkandarasi ni kukamilisha sehemu hiyo kabla ya mwisho wa Desemba mwaka huu, akieleza kuwa hadi sasa asilimia 70 ya kazi za ujenzi wa tuta na maandalizi ya udongo (earthwork) zimekamilika.
Amesema kazi ya uwekaji wa tabaka la kwanza la barabara (C1) tayari imeanza, ambapo sehemu 12 zimekamilishwa, huku mkandarasi akilenga kukamilisha kazi zote za earthwork ndani ya siku 40 zijazo.
Mhandisi Huang amesema baada ya kukamilika kwa kazi hizo, uwekaji wa tabaka za barabara utaendelea kwa kasi kuanzia mwishoni mwa Novemba, akieleza kuwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu wanatarajia kukamilisha sehemu kubwa ya mradi.
Akizungumzia upande wa Moshono, amesema mkandarasi tayari amepeleka vikosi viwili vya ujenzi katika eneo hilo na kazi zinaendelea, huku takribani asilimia 30 ya kazi za earthwork ikiwa tayari imekamilika.

