NA DENIS MLOWE, IRINGA
MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGOs) mkoani Iringa yameeleza umuhimu wa kujenga mtandao wa pamoja utakaowezesha mashirika hayo kufahamiana, kubadilishana huduma na taarifa, pamoja na kupunguza urudiaji wa miradi katika maeneo mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa NaCoNGO Fidelis Filipatali, wakati akizungumza na wanahabari katika kliniki ya NGOs inayofanyika kwa siku mbili katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ambapo mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka maeneo mbalimbali yalikutana kwa ajili ya kutambulishana na kujadili namna ya kuimarisha shughuli zao.
Filipatali alisema licha ya kuwa na maonyesho ya shughuli wanazofanya pia kiliniki hiyo imeleta pamoja mashirika mbalimbali ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakifanya shughuli katika maeneo tofauti bila kuwa na fursa ya kutosha ya kufahamiana, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya ubunifu wa NaCoNGO Mkoa wa Iringa katika kuimarisha ushirikiano na uendelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Tumekuja na ubunifu huu kama kaulimbiu ya mwaka huu ya kutaka mashirika yote yasiyo ya kiserikali yaweze kujitegemea na kuwa wabunifu ubunifu mmoja wapo ni kutengeneza one stop centre ya wadau wote wa mashirika yasiyo ya kiserikali wakae pamoja, waone wanatekeleza shughuli zipi, wako wapi na wanafanya nini,” alisema.
Alisema jumla ya mashirika 186 yameweza kushiriki katika kongamano hilo, hali ambayo imewezesha mashirika makubwa na madogo kukutana, kutambuana na kuona namna yanavyoweza kushirikiana katika utekelezaji wa miradi.
Filipatali alisema kuwa mfumo huo pia utasaidia kupunguza hali ya mashirika kutekeleza miradi inayofanana katika eneo moja huku maeneo mengine yakikosa huduma, kwa kuwa mashirika yatakuwa na taarifa za shughuli zinazotekelezwa na wenzao.
“Miradi isiwe duplicated, isiwe inakuwa mingi sehemu moja. Kikubwa zaidi tunatengeneza mtandao hapa, hawa wanafahamiana kwamba bidhaa hii inaweza kupatikana hapa na nyingine inaweza kupatikana sehemu nyingine,” alisema.
Aliongeza kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanafanya shughuli katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, mazingira, elimu na maji, hivyo mtandao huo utatoa fursa kwa mashirika yanayozalisha bidhaa au huduma mbalimbali kushirikiana na yale yenye mahitaji ya bidhaa hizo.
Filipatali alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza uwezo wa mashirika kujitegemea kiuchumi, badala ya kutegemea wafadhili pekee katika utekelezaji wa miradi yao kwani kwa muda mrefu mashirika mengi yamekuwa yakiandaa miradi na kuiwasilisha kwa wafadhili kwa ajili ya kupata fedha za utekelezaji, lakini kupitia mikutano na makongamano kama hayo, mashirika yanaweza kuunganisha bidhaa na huduma wanazozalisha na kuwa sehemu ya miradi inayotekelezwa katika mkoa.
“Tunataka tusitegemee tu wafadhili. Huku nyuma tumekuwa tukiandika miradi na kupeleka kwa wafadhili, lakini kupitia makongamano kama haya yatatuweka pamoja kuwa na bidhaa tunazozalisha ziwe sehemu ya miradi inayofanyika hapa mkoani,” alisema.
Aidha, alisema NaCoNGO inaamini kuwa ubunifu na uendelevu wa miradi ya mashirika hayo utategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano unaojengwa kupitia mikutano hiyo, huku akisisitiza kuwa mpango huo hautaishia katika ngazi ya Mkoa wa Iringa pekee.
Alisema mpango huo utaendelea katika wilaya mbalimbali, ikiwemo Mufindi, ambako kuna mpango wa Mufindi Investment and Expo utakaowakutanisha mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau wengine kwa ajili ya kuonesha bidhaa na huduma zinazozalishwa na mashirika hayo.

