Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Uislamu unahimiza upendo, amani, umoja na mshikamano, misingi ambayo ni muhimu katika kujenga jamii yenye utulivu, maelewano na maendeleo.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 4 Oktoba 2026, katika muhadhara wa Kiislamu ulioandaliwa na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar na kufanyika Masjid Jamiu Zinjibar, Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alhaj Dkt. Mwinyi amesema umoja huimarisha jamii, huondoa migawanyiko na chuki na kuwawezesha wananchi kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Amewataka waumini kuendelea kuzingatia mafundisho mema ya dini, ikiwemo kuheshimiana, kusaidiana, kusameheana na kudumisha amani, akieleza kuwa maadili hayo yana nafasi kubwa katika kujenga familia na jamii imara.
Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema ujio wa Masheikh kutoka nje ya nchi ni fursa muhimu kwa waumini kupata elimu na nasaha kuhusu maisha ya Kiislamu, maadili, upendo na mshikamano, hivyo amewahimiza kuyasikiliza na kuyafanyia kazi mawaidha yenye manufaa katika maisha yao ya kila siku.
Ameipongeza Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa juhudi zake za kutoa elimu ya dini na kuhamasisha amani, upendo na mshikamano katika jamii, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwafikishia wananchi mafundisho yanayojenga maadili mema.
Alhaj Dkt. Mwinyi amewataka waumini kufuata yale yaliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu katika Qur’ani Tukufu na mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W.), huku wakijiepusha na mambo yanayoweza kuleta chuki, migawanyiko na kuvuruga amani.
Naye Mufti Ismail Menk kutoka Zimbabwe ameipongeza Zanzibar kwa kuendelea kudumisha upendo, mshikamano na maadili mema katika jamii, akisisitiza kuwa umoja na amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.
Muhadhara huo umewakutanisha viongozi na wananchi mbalimbali, ambao wamepata fursa ya kusikiliza mawaidha kutoka kwa Masheikh kuhusu umuhimu wa kushikamana na mafundisho ya dini, kudumisha amani, upendo na kuheshimiana katika jamii.

