“Awataka wasikae ofisini watatue kero za wananchi.”

Na Happy Lazaro, Arusha .

Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Gabriel Makalla, amewataka Wakuu wapya wa Wilaya za Ngorongoro, Arumeru na Arusha walioapishwa leo kuhakikisha Ofisi za Umma zinakuwa kimbilio la wananchi kwa kusikiliza na kushughulikia kero zao kwa wakati, akisema hatua hiyo ni sehemu ya kutekeleza ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuacha tabasamu kwa wananchi.

CPA Makalla amesema wananchi wanapofika katika Ofisi za Serikali wanapaswa kuona kuwa kero zao zimepokelewa, kusikilizwa na kuchukuliwa hatua, akisisitiza kuwa viongozi hawapaswi kulea migogoro wala madukuduku ya wananchi.

CPA Makalla amesema Mkoa wa Arusha una nafasi muhimu kiuchumi, kidiplomasia na katika sekta ya utalii, hivyo amewataka kusimamia kwa ufanisi maeneo hayo, ikiwemo kuhakikisha malango ya Mkoa yanakuwa safi na kuvutia wageni na watalii wanaofika Mkoani hapa kupitia Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro KIA na wale wanaotoka kupitia Wilayani Arumeru.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Arusha Mjini Mhe. Paul Christian Makonda, amewapongeza Wakuu hao wa Wilaya na kumshukuru Mhe. Makalla kwa uongozi, malezi yake na usimamizi wa miradi ya maendeleo, akisema uwepo wake Arusha umeongeza ujasiri kwa viongozi katika kuwahudumia wananchi huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa Bw. Ole Thomas Sabaya akisisitiza umuhimu wa viongozi kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi.

Viongozi walioapishwa leo ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Nicodemus Tambo Mwikozi, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Neema Kichiki Lugangira na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Luteni Kanali Robert Augustino Kakowangile ambapo CPA Makalla ametumia nafasi hiyo pia kuwashukuru watangulizi wao kwa uongozi na utumishi wao katika Mkoa wa Arusha.

Katika uapisho huo Mkuu wa Mkoa alishuhudia pia Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Halmashauri ya Longido Winfrid Erneus Tamba akiungana na Wakuu hao wapya wa Wilaya kula kiapo cha maadili.