Serikali imesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuwa kiungo kati yake na wananchi katika kutoa elimu kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025, fursa zinazotokana na sera hiyo na namna wananchi wanavyoweza kushiriki katika utekelezaji wake.

Wito huo umetolewa mkoani Morogoro na Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba, wakati wa mafunzo kwa wahariri, waandishi wa habari na wamiliki wa mitandao ya kijamii, yaliyolenga kuongeza uelewa kuhusu sera hiyo na kuwajengea uwezo wa kuhabarisha umma kwa usahihi.

Haraba amesema kuzinduliwa kwa sera ni hatua ya mwanzo, huku utekelezaji wake ukihitaji mikakati, miongozo, sheria, kanuni na taratibu zitakazowezesha kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa.

Aidha, amewataka wananchi kufuatilia utekelezaji wa sera hiyo na kutoa mrejesho pale wanapobaini changamoto, huku Serikali ikiendelea kushirikiana na wadau wa habari kwa kutoa taarifa na ufafanuzi unaohitajika.

Amesema lengo ni kuhakikisha taarifa kuhusu sera hiyo zinawafikia wananchi wa ngazi zote na kuwawezesha kuelewa mwelekeo wa Serikali, fursa zilizopo na namna ya kushiriki katika maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii, Ndugu Mathias Canal, amewataka waandishi wa habari kutumia ujuzi walioupata kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 kuelimisha umma kuhusu fursa na manufaa yanayopatikana kupitia utekelezaji wa sera hiyo.

Amesema waandishi wanapaswa kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi kwa kutoa taarifa sahihi, zenye kina na zinazolenga kujenga uelewa wa jamii.

Canal amesema sera hiyo inaweza kutoa fursa kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani, huku ikichochea uwazi, ufanisi na maendeleo ya uchumi.

Ameongeza kuwa waandishi wanapaswa kuchambua kwa kina masuala yanayohusu Serikali na kuyafikisha kwa wananchi kwa lugha inayoeleweka, badala ya kuishia katika kuripoti taarifa bila kuangalia athari na manufaa yake kwa jamii.

Aidha, amewataka waandishi kuzingatia uhakiki wa ukweli na kushirikiana na maafisa habari wa Wizara ya Fedha pamoja na wataalamu mbalimbali ili kupata taarifa sahihi.

“Tufanye kazi kubwa ya uhakiki wa ukweli,” amesema Canal, akisisitiza kuwa mawasiliano na wataalamu na viongozi wanaohusika na sera hiyo ni muhimu katika kujenga habari zenye weledi.

Katika mafunzo hayo, waandishi walipata uelewa kuhusu tofauti kati ya dira, sera, sheria, kanuni na mwongozo, pamoja na uhusiano kati ya Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Mafunzo hayo yalitolewa na wataalamu, akiwemo Dk. Maige Makaseke Mwasimba kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe na Dk. Hezron Makundi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Canal amesema waandishi wanapaswa kutumia mafunzo hayo kama chachu ya kuandika habari zinazowajibika kwa jamii na zinazosaidia wananchi kuelewa masuala ya usimamizi wa mnyororo wa ugavi.

Amesema taarifa hizo zinapaswa pia kuonesha fursa zilizopo kwa wananchi na wafanyabiashara wa ndani, pamoja na umuhimu wa sera hiyo katika shughuli za Serikali na uchumi wa taifa.

Amesisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuendelea kulinda maadili ya taaluma, kufanya uchambuzi wa kina na kuhakikisha taarifa wanazotoa zina ukweli na weledi.

“Tukayatumie mafunzo haya kama chachu ya kuandika habari zenye weledi, msingi wake uwe ni uwajibikaji kwa jamii yetu,” amesema Canal