Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amekabidhi ofisi kwa Mkurugenzi mpya, Warda Abeid Maulid, akiwa ameiacha Manispaa hiyo ikiwa na zaidi ya Sh bilioni 16 benki, hali inayoonesha kuwa ina ukwasi mkubwa na uwezo mzuri wa kifedha.

Shemwelekwa amesema tangu alipoingia katika Halmashauri ya Kibaha Mjini, makusanyo ya mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 7 mwaka 2024/2025 hadi kufikia Sh bilioni 18, sawa na ongezeko la Sh bilioni 11.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba 30, Manispaa tayari imefikia asilimia 50 ya makusanyo, huku akieleza kuwa anaamini Mkurugenzi mpya ataendeleza kasi hiyo na kufikia malengo yaliyowekwa.

Ameongeza kuwa Manispaa imejiwekea lengo la kukusanya Sh bilioni 30 ifikapo 2030, sambamba na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato katika eneo lenye ukubwa wa ekari 26, ambako Sh bilioni 1.18 zimetengwa kwa ajili ya maegesho ya magari, kituo cha mafuta na shughuli nyingine za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi , Warda Abeid Maulid, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kuahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kushirikiana na watumishi katika kuendeleza maendeleo ya Manispaa hiyo.

Naye Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, amesema matarajio ni kuwa Warda ataongeza chachu ya maendeleo kwa wananchi, huku akimpongeza Shemwelekwa kwa mchango wake katika kuongeza mapato na kuimarisha Manispaa hiyo.