Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, ametoa maelekezo sita kwa wadau watakaohusika na utekelezaji wa programu ya kuwezesha kampuni changa za TEHAMA, akisisitiza mikopo ya Shilingi bilioni 5 iliyotengwa na Serikali itumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kuleta matokeo yanayoonekana katika kukuza biashara za vijana nchini.

Ametoa maelekezo hayo Oktoba 2, 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji kwa ajili ya kusaidia kampuni changa zinazomilikiwa na vijana kupata mitaji ya kukuza ubunifu na biashara zao.

Katika maelekezo hayo,Mhe. Kairuki amewataka wabunifu na kampuni changa zote zinazolengwa na programu hiyo kujisajili katika Mfumo wa Jamii Hunt, ambao ni mfumo rasmi wa utambuzi na uwasilishaji wa maombi, huku akisisitiza maombi kushughulikiwa kwa ufanisi baada ya uchambuzi kukamilika.

Aidha, ameitaka Tume ya TEHAMA kukamilisha mwongozo utakaowezesha kampuni changa za TEHAMA kushiriki katika zabuni za Serikali na kuwasilisha suala hilo kwa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa hatua stahiki. Pia ameitaka Wizara kwa kushirikiana na Tume ya TEHAMA na Benki ya Azania kuweka mfumo wa kupima matokeo ya programu hiyo kwa kuzingatia ukuaji wa kampuni, ajira, mauzo, masoko, bidhaa na huduma mpya pamoja na urejeshaji wa mikopo.

Katika maelekezo mengine, amewataka wabunifu kutafakari umuhimu wa kuanzisha umoja wao rasmi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili kurahisisha uwakilishi wao, utambuzi wa changamoto na ubainishaji wa mahitaji yao kwa wakati. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuandaliwa mpango wa elimu kwa umma utakaowawezesha wabunifu na kampuni changa kuelewa vigezo, utaratibu wa maombi, wajibu wa wanufaika na manufaa ya programu hiyo.

Ameelekeza pia kuwa watakaopata mikopo hiyo wanapaswa kuitumia kwa madhumuni yaliyokusudiwa, kukuza biashara zao, kutafuta masoko ndani na nje ya nchi na kuchangia kukuza sekta ya TEHAMA ya Tanzania katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Amebainisha kuwa mikopo hiyo itatolewa katika makundi matatu kulingana na mahitaji ya biashara, ambapo mkopo mdogo ni kuanzia Shilingi milioni 1 hadi milioni 25, mkopo wa kati ni zaidi ya milioni 25 hadi milioni 100, huku mkopo mkubwa ukiwa zaidi ya milioni 100 hadi milioni 500. Amesisitiza kuwa mafanikio ya programu hiyo hayatapimwa kwa kiasi cha fedha kilichotolewa pekee, bali pia ukuaji wa kampuni, ajira zitakazozalishwa, ongezeko la mauzo na mapato pamoja na upanuzi wa masoko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dkt. Esther Mang’enya, amesema benki hiyo kwa kushirikiana na Wizara itasimamia tathmini na utoaji wa mikopo kwa kampuni zitakazokidhi vigezo, huku akibainisha kuwa ushirikiano huo utajumuisha pia kuwajengea vijana uwezo katika usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu na mipango ya biashara ili kujenga kampuni endelevu zitakazozalisha ajira.

Naye, Mwakilishi wa Tanzania Startups Association (TSA), akizungumza pia kwa niaba ya Zanzibar Startups Association, amewataka wabunifu na kampuni changa kutumia vizuri fursa ya mikopo hiyo na kuhakikisha wanarejesha fedha ili kuwawezesha wabunifu wengine kunufaika, huku akisisitiza kuwa matumizi sahihi ya mfuko huo yataongeza uaminifu kwa Serikali na kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya TEHAMA. Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi kwa kampuni changa.