Na Mwandishi wetu, Geita

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Martine Shigela, ameusifu Mkoa wa Geita, kwamba ni moja ya kituo chake cha kazi alichowahi kuhudumu akiwa na wasaidizi waliofanya naye kazi kwa umoja katika kufanikisha maendeleo mbalimbali kwa wananchi.

RC Shigela ameeleza hayo katika tafrija ya kuagwa rasmi Mkoani Geita alipofanya kazi kwa miaka mitano na kwenda Mkoani Manyara na kukaribishwa kwa RC mpya wa Geita, Alexander Pastory Mnyeti iliyofanyika manispaa ya Geita.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Manyara, ametolea mfano wa maonesho ya kitaifa ya teknolojia ya madini ambayo mwaka huu wa 2026 ni ya tisa yanayofanyika viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan manispaa ya Geita, ambayo anajivunia kuona yakizidi kukua na kupiga hatua..

Amesema wakati anaingia Mkoa wa Geita, makusanyo ya fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo kufadhili maonesho hayo ikiwemo ujenzi wa vibanda, ilikuwa kati ya Sh 50 milioni hadi Sh100 milioni ambapo kupitia ushirikiano na wadau wa maendeleo pamoja na wasaidizi wake, ameacha makusanyo yakiwa zaidi ya Sh 1.4 bilioni.

“Natoa wito kwa RC Mnyeti kuendeleza vyema pale nilipoishia ili maonesho hayo yazidi kuwa ya kisasa zaidi kunufaisha wananchi mbalimbali,” amesema RC Shigela.

RC Shigela anaondoka Geita baada ya miaka minne alipoingia akitokea mkoani Tanga akichukua nafasi ya Rosemary Senyamule aliyehamishiwa Dodoma katika mabadiliko yaliyofanyika Agosti 2022.

RC Shigela kwa kiasi kikubwa amesaidia kukua kwa uchumi wa mkoa huo, kwa kufanyika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya, elimu, l na miundombinu ya barabara ikipiga hatua.

Kwa upande wake, RC wa Geita, Alexander Mnyeti ameeleza kuwa ataendelea kushirikiana na RC Shigela kwa kumuomba ushauri katika kipindi chake cha uongozi Mkoani Geita.

RC Mnyeti amesema uzoefu wa mtangulizi wake RC Shigela unaweza kumsaidia katika kuendesha mkoa huo katika uongozi wake kwa sasa.

RC Mnyeti ameuomba viongozi na wananchi wa Geita kumpokea na kushirikiana naye katika kuujenga Mkoa huo huku akitoa rai kwa viongozi wa dini kumwombea mtangulizi wake kwenye kutuo chake kipya.

“Ndugu zangu huu ni mtumbwi, hivi sasa mimi Mnyeti ndiyo nahodha wenu, naomba mnipokee, kwa wale ambao mnaonichukia, mnipende tuchape kazi tuijenge Geita yetu nzuri.” amesema RC Mnyeti.