Tume ya Ushindani (FCC) imewahimiza wafanyabiashara, hususan kampuni za wazawa, kusajili nembo za biashara na kuhakikisha zinafuatilia bidhaa zao sokoni ili kusaidia kudhibiti bidhaa bandia nchini.

Rai hiyo imetolewa wakati FCC ilipotoa mafunzo kuhusu masuala ya ushindani kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini, ikiwa ni sehemu ya Siku Maalum ya “Made in Tanzania” katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita.

Kupitia siku hiyo, wazalishaji na watoa huduma walipata elimu kuhusu wajibu wao katika kudhibiti bidhaa bandia kwa kushirikiana na Serikali kupitia FCC.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Nsajigwa Wilfred, Afisa Uhusiano wa Umma Mkuu wa FCC, amesema walaji wanapaswa kuepuka kununua bidhaa zenye nembo za kughushi au zinazoweza kuwadanganya.

Amesema mlaji anapaswa kuwa makini wakati wa kununua bidhaa kwa kuangalia alama au nembo ya bidhaa, anuani ya mzalishaji pamoja na nchi ambako bidhaa hiyo imetengenezwa.

“Pale ambapo bidhaa haina vitu hivyo vitatu, mlaji hapaswi kununua bidhaa hiyo,” amesema Nsajigwa.

Aidha, amewataka walaji kutoa taarifa kwa FCC kwa ajili ya kupata ushauri na msaada pale wanapobaini bidhaa waliyonunua imeshindwa kufanya kazi iliyokusudiwa.

Kwa upande wa wafanyabiashara, hususan watengenezaji, wasambazaji, waingizaji, wapitishaji wa bidhaa – (transit and transhipment) na wauzaji, Nsajigwa amesema wanapaswa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Alama za Bidhaa kwa kuhakikisha wanatengeneza, kusambaza, kuingiza na kuuza bidhaa halisi zenye utambulisho unaokidhi matakwa ya kisheria.

Amesema wamiliki wa alama za biashara – (brand owners), wanapaswa kuchunguza na kufuatilia bidhaa zao sokoni ili kubaini iwapo kuna watu wanaouza bidhaa bandia zinazotumia alama zao.

Kwa mujibu wa Nsajigwa, wamiliki wa alama za biashara wanapaswa kuwasilisha malalamiko FCC mara wanapobaini kuwepo kwa bidhaa zinazoghushiwa au kutumia alama zao bila uhalali.

“Tunasisitiza na ni muhimu kwa wenye kumiliki alama au nembo za biashara – (brand owners), waelewe kwamba wahalifu wanaotengeneza bidhaa bandia ni washindani wao wasioonekana (unseen competitors). Hivyo, wanapaswa kuwa na bajeti ya kutosha na kujipanga vizuri katika kukabiliana nao kwa kushirikiana na FCC, kama ambavyo wanavyowakabili washindani wanaoonekana kupitia matangazo mbalimbali ya kuvutia walaji,” amesema Nsajigwa.

Nsajigwa amewahimiza wadau wote wa sekta ya biashara na madini kutimiza wajibu wao katika kudhibiti bidhaa bandia na kuzingatia sheria, taratibu na misingi ya ushindani katika kufanya biashara.

Amesema juhudi za pamoja za Serikali, wafanyabiashara, wazalishaji, wasambazaji na walaji ni muhimu katika kuhakikisha soko linakuwa na bidhaa salama na halali.

“Tanzania bila bidhaa bandia inawezekana pale ambapo kila mdau katika nafasi yake atatimiza wajibu wake,” amesema.