Na WMA – GEITA
Banda la Wakala wa Vipimo (WMA) limekuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Mkoani Geita, baada ya mamia ya wanafunzi kuendeleq kufurika kujifunza elimu ya matumizi sahihi ya vipimo.
Wanafunzi hao kutoka shule mbalimbali za Geita wameonesha shauku kubwa ya kutaka kufahamu jinsi vipimo vinavyolinda haki zao kama walaji, hususan katika ununuzi wa bidhaa za kila siku kama vile gesi ya kupikia, mafuta na hata mizani inayotumika masokoni na madukani.
Akizungumza na wanafunzi hao, Meneja wa WMA Mkoa wa Mara Bw. Balisco Kapesa, ambaye ni mmoja wa Watumishi wa WMA walioko katika maonesho hayo, aliwasisitiza wanafunzi kuwa na utamaduni wa kuhoji na kujiridhisha kama kifaa cha kupimia kimehakikiwa na WMA kabla ya kununua bidhaa yoyote, huku akiwaonesha kwa vitendo jinsi ya kutambua stika halali ya WMA kwenye mizani.
Kwa upande wake, Mwalimu wa wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Zanzui ambayo ni moja ya shule zilizotembelea banda la WMA hao, Mwl. Sofia Kayongo alisema elimu hiyo ya vipimo ni ya vitendo na inapaswa kuingizwa kwenye mitaala ya shule, kwani inamjengea mwanafunzi uwezo wa kuwa mjasiriamali mwadilifu na mlaji makini, badala ya kusoma nadharia tu darasani.
Mmoja wa wanafunzi, Blasius Enosy, alisema elimu aliyoipata ni muhimu sana kwake na kwa familia yake, kwani sasa amejua kuwa kama mtungi wa gesi haujapimwa kwenye mzani uliohakikiwa na WMA, basi haupaswi kununuliwa, kwa kaulimbiu isemayo “Kama Gesi Haijapimwa kwenye mzani uliohakikiwa na WMA, Siitaki!”
Kwa ujumla, Maonesho ya Madini Geita 2026 yamekuwa fursa muhimu kwa WMA kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, huku kaulimbiu ya Wakala isemayo “Kipimo Sahihi ni Haki Yako” ikiendelea kusikika kwa wananchi wengi wanaotembelea banda hilo.
WMA inaendelea na utaratibu wa kufikisha elimu ya vipimo kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi ambapo inatekeleza Mpango wa kuanzisha na kuendesha Klabu za Vipimo mashuleni.

