MPANDA, KATAVI:
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imesema imejiridhisha na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluh Hassan katika ujenzi wa miradi ya Umwagiliaji na kutokana na kazi hiyo haitakubali kukaa kimya bila kupaza sauti kutetea maslahi ya wakulima.
Kamati hiyo imesema fedha zilizotumika katika miradi hiyo na mabadiliko yaliyofanywa na Serikali ya Dkt. Samia Suluh Hassan ni matokeo ya miradi kufanya vizuri na miradi inapofanya vizuri maneno ni lazima yawepo.
Akizungumza Mkoani Katavi katika ziara ya siku Tano ya kamati hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Mhe. Deodatus Philip Mwanyika amesema wamejionea kazi kubwa na nzuri inayofanywa katika mradi wa Umwagiliaji Mwamkulu.
“Ukweli usemwe na hatutakubali kukaa kimya na kufunga midomo hii miradi hii kwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia ni lazima kuonekana na mahali panapofanya vizuri na kukaonekana maneno ni lazima”, Amesema
“Kilimo kilikuwepo tangu wakati huo na kauli mbiu ilikuwa Kilimo ni Uti wa Mgongo, lakini Rais Samia kaja kutafsiri na kuonekana Kilimo kweli ni uti wa mgongo, hii miradi ya Umwagiliaji inaenda kugusa wakulima na wananchi moja kwa moja na hatutasita kuwasemea pale inapofanya vizuri,”ameongeza
Amehimiza kuwa “Mradi huo wa shilingi bilioni 33.9, uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, unaenda kubadilisha maisha ya wakulima wa Mwamkuru kutoka kwenye adha ya miaka mingi na kuwaletea ukombozi wa kiuchumi,”amesisitiza.
Mwanyika ameeleza kuwa utekeleza wa mradi umefikia asilimia 83, ambapo mfereji mkuu wa maji wa kilomita 7.7 umekamilika kwa asilimia 100, mifereji mingine mikuu mitatu ya kilomita 14 imekamilika, barabara za mashambani za kilomita 35 na mifereji ya kurudisha maji Mto Katuma ya kilomita 18 zimekamilika. Pia, ghala la nafaka la tani 4,000 limefikia zaidi ya asilimia 90 ili kuondoa upotevu wa mazao baada ya kuvuna.
Amesisitiza kuwa wakati Tanzania ikijiwekea malengo ya kulisha Dunia Katavi ni mkoa wa kimkakati katika uzalishaji hususani wa mazao ya mpunga na mahindi hivyo wananchi wapokee miradi hiyo na kuitunza.
Naye. Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amebainisha kuwa Mkoa wa Katavi ambao unategemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 95 umepokea takriban trilioni 1.4 katika sekta mbalimbali na bilioni 70 kwenye Umwagiliaji pekee. Amesisitiza kuwa Mwamkuru ni hatua kubwa ya mafanikio ya kilimo cha Umwagiliaji na kuomba mabonde mengine mkoani humo nayo yaendelezwe ili kuwa na kilimo chenye tija.
Akizungumzia thamani ya mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuph, amesema mradi huo umeleta matumaini makubwa kwa wananchi na utaongeza mapato ya Halmashauri.
Amesema kuwa Wilaya imewashirikisha viongozi wa dini, wazee, vijana wa bodaboda na vyama vya siasa kujionea uwekezaji huo wa serikali, huku akiomba kukamilishwa kwa bwawa la hifadhi ya maji ili wananchi walime mara mbili kwa mwaka.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Umwagiliaji na Zana za Kilimo), Eng. Athuman Kilundumya, ameahidi kuwa Tume itaendelea kushirikiana na Jamii katika kuleta matokea chanta ya miradi hiyo na Wizara itaendelea kuiwezesha taasisi hiyo ili kufikia lengo la Serikali.
Akitoa ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa mbegu Kilundumya ameitaka Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kuhakikisha wanaweka kambi katika eneo la mradi wa Umwagiliaji Mwamkulu ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakulima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amebainisha kuwa mikataba ya Tume haina gharama za riba (interest), hatua iliyowezesha Serikali kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 28 ambazo zingelipa riba.
Mndolwa amesisitiza kutokana na athari za Elnino zinazotarajiwa kutokea hivi karibuni, Tume imemuelekeza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anamaliza kwa wakati na kwa ubora kazi za mashambani kwanza kabla ya majengo ya utawala ili kujikinga na madhara yanayoweza kutokea.
Pia amesema Tume ipo kwenye mchakato wa kupata mashine zitakazofungwa kwenye ghala la mpunga lililojengwa katika mradi huo ili wananchi waweze kuchakata mazao yao, huku akishukuru ushirikiano wa mkoa na wilaya katika kutoa elimu na kusimamia ukusanyaji wa tozo za Ada za Umwagiliaji.
Kwa niaba ya Mwenyekiti wa skimu na wakulima wa katika skimu hiyo, Mzee Boniphace Chidesela, ameleza kwa hisia kuwa kabla ya mradi walitumia masaa manne hadi matano kufika shambani na kulipia shilingi 10,000 kusafirisha gunia moja la mazao. Hata hivyo, hivi sasa magari yanafika hadi shambani, gharama imeshuka hadi shilingi 1,000 na safari inachukua dakika 15 tu.
Uwekezaji huu unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka gunia 20 hadi 35–40 kwa hekari, huku ukiongeza wanufaika kutoka 300 hadi 1,500.
Akihitimisha ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Mbunge wa Njombe Mjini, Mhe. Deodatus Mwanyika, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka nguvu kubwa kwenye kilimo na kubainisha kuwa mradi huo unaonyesha thamani halisi ya fedha za umma (Value for Money).

