Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenye akizungumza kwenye ziara hiyo jijini Arusha

Happy Lazaro, Arusha.

Arusha.Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenye, amewataka wananchi jijini Arusha kushirikiana na Serikali katika kulinda njia za maji, akisisitiza kuwa uamuzi wa mtu mmoja kuzuia au kugeuza mkondo wa maji unaweza kuathiri jamii nzima na kusababisha uharibifu wa miundombinu.

Kasekenye ametoa kauli hiyo leo jijini Arusha baada ya kukagua miradi mbalimbali ya barabara na miundombinu inayoboreshwa na Serikali katika maandalizi ya Michuano ya AFCON, akieleza kuwa maandalizi hayo yanapaswa kwenda sambamba na hatua za kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa.

Amesema suala la maji linahitaji ushirikiano wa wananchi na viongozi wa Serikali za Mitaa, kwa kuwa kuzuia maji katika njia zake za asili kunaweza kuyafanya kuelekea maeneo mengine na kusababisha madhara kwa barabara, madaraja pamoja na makazi ya watu.

“Unapozuia maji kwenye mkondo unahatarisha shughuli zote za Watanzania, siyo za kwako. Tunaomba wananchi tushirikiane na viongozi wetu, hasa watendaji wa kata na vijiji, kuhakikisha maji yanaelekezwa kwenye mikondo yake,” amesema.

Kwa mujibu wa Kasekenye, juhudi za mtu mmoja kujikinga na maji zinaweza kuhamisha tatizo kwenda kwa wananchi wengine, hivyo kila mmoja anapaswa kutambua kuwa usalama wa miundombinu na mazingira ni jukumu la pamoja.

“Unaweza kujilinda wewe mwenyewe kwa kupeleka maji upande mwingine, lakini ukaleta madhara mengi sana kwa watu wengine. Kwa hiyo ni muhimu kila mmoja kuona suala hili ni jukumu lake,” amesema.

Amesema wananchi wanapaswa kutumia muda huu kufanya usafi wa mifereji na kuchukua hatua za kuhakikisha maji yana njia ya kupita, hatua ambayo itasaidia kupunguza hatari ya mafuriko na uharibifu unaoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa.

Katika hatua nyingine, Kasekenye amesema TANROADS Kanda ya Kaskazini imejiandaa kukabiliana na uharibifu wa miundombinu unaoweza kutokea kutokana na mvua, ikiwamo kuweka vifaa vya dharura ambavyo vinaweza kutumika mara moja endapo barabara au daraja vitapata hitilafu.

Amesema uwepo wa vifaa hivyo utasaidia Serikali kuchukua hatua kwa haraka katika kurejesha huduma pale miundombinu inapoharibika, badala ya kusubiri maandalizi mapya ya vifaa baada ya tukio kutokea.

“Wenzetu wa TANROADS wameshachukua vifaa ambavyo tunategemea. Kama daraja likianguka leo, tayari tuna stock ya vifaa ambavyo vinaweza kupelekwa. Kama vinatakiwa vifaa vya chuma, tayari tunavyo,” amesema.

Ameeleza kuwa vifaa hivyo vimeandaliwa na kuwekwa katika maeneo mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya dharura, ili kurahisisha upatikanaji na usafirishaji wake pale majanga yanapotokea.

Kasekenye amesema tahadhari hiyo ni muhimu hasa katika maeneo yanayoweza kukumbwa na mvua nyingi, akitaja Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuwa miongoni mwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini inayohitaji maandalizi ya kutosha.

Amesema maandalizi ya Serikali hayalengi barabara pekee, bali yanahusisha pia mifumo ya kukabiliana na majanga ili kuhakikisha athari zinapojitokeza zinadhibitiwa kwa wakati na huduma muhimu zinaendelea.

“Serikali kupitia mifumo yake ya kukabiliana na maafa, ikiwemo uratibu unaofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, imeendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na majanga yatakayotokea,” amesema.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi, Serikali za Mitaa na mamlaka zinazohusika na miundombinu ni muhimu katika kuzuia madhara ambayo yanaweza kuepukika, hasa katika kipindi ambacho maandalizi ya kukabiliana na mvua yanaendelea.