*Kufanya Utafiti wa Kina wa madini*
*Kuimarisha upatikanaji wa taarifa za madini
Pori, Finland
Tanzania na Finland zimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika utafiti wa madini baada ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia ya Finland (GTK) kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) unaolenga kuimarisha utafiti wa jiolojia na upatikanaji wa taarifa sahihi za rasilimali za madini nchini.
Ushirikiano wa Tanzania na Finland unaendeleza MoU iliyoingiwa mwaka 2024 yenye lengo la kuongeza uwezo kwa wataalam wa Tanzania na kuimarisha upatikanaji wa taarifa za kisayansi zitakazosaidia katika utafiti, uendelezaji na uongezaji thamani katika rasilimali madini
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alisema kuwa, Serikali ya Tanzania inathamini ushirikiano huo kwa kuwa una fursa ya kuimarisha uwezo wa Tanzania katika kutambua, kuchambua ili kutambua kiwango cha rasilimali madini zilizopo nchini.
Aliongeza kuwa, taarifa sahihi za kijiolojia ni msingi muhimu katika kufanya tafiti, kupanga matumizi ya rasilimali na kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini.
“ Ushirikiano huu utaleta mabadiliko katika namna Tanzania inavyokusanya, kuchambua na kutumia taarifa za kijiolojia,” alisema Mbibo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GTK, Dkt. Saku Vuori, alisema utekelezaji wa programu ya kuwajengea uwezo wataalam wa GST tayari imeanza, huku wataalam wa GTK wakiendelea kufanya tathmini ya hatua nyingine za utekelezaji.
Dkt. Vuori alisema kuwa, GTK pia iko tayari kuiwezesha GST katika kuimarisha uwezo wa Maabara mpya inayojengwa Dodoma, ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya teknolojia ya kisasa kwa ajili ya uchambuzi na upimaji wa sampuli za miamba na madini.
Hatua hiyo inalenga kuiwezesha Tanzania kupata taarifa za maabara zinazokidhi viwango vya kisasa, ambazo zinaweza kutumika katika utafiti, tathmini ya rasilimali madini na maamuzi ya uwekezaji.
Katika makubaliano hayo, Umoja wa Ulaya (EU) umeonesha nia ya kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa ushirikiano huo, hususan katika kuhakikisha taarifa na takwimu za kijiolojia zinazokusanywa zina ubora na sahihi kwa uwekezaji.
Pamoja na mambo mengine, ujumbe wa Tanzania ulipata fursa ya kutembelea maabara ya kisasa ya GTK na kupata maelezo kuhusu matumizi ya teknolojia katika uchambuzi wa sampuli za miamba na madini pamoja na mifumo ya uhakiki na udhibiti wa ubora wa taarifa za kisayansi.
Ziara hiyo imehusisha wajumbe kutoka Wizara ya Madini, GST, Chemba ya Migodi Tanzania, kampuni za uchimbaji madini, Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Ubalozi wa Finland nchini Tanzania.

