📍 DODOMA 

Mtaalamu wa Afya kutoka kituo Cha Afya Mkonze, Dkt. Ngosha Emily, amewataka vijana waliopata ufaulu wa chini kubadili mtazamo kuhusu mafanikio na kutambua kuwa shahada ya kwanza siyo njia pekee ya kupata ajira na kujenga maisha.

Akizungumza Oktoba mosi 2026 Jijini Dodoma na Fullshangwe Blog, Amesema baadhi ya vijana wanaomaliza elimu ya sekondari na vyuo wamejenga dhana kwamba bila shahada hawawezi kufanikiwa, hali inayowafanya waliopata matokeo ya chini, ikiwemo GPA chini ya 3.0, kukata tamaa.

Dkt. Ngosha amesema thamani ya mtu kazini haipaswi kupimwa kwa kiwango cha shahada pekee, bali pia uwezo, ujuzi na matokeo anayoyazalisha katika eneo lake la kazi.

Amesema wapo wataalamu wengi nchini wanaofanya vizuri wakiwa na elimu ya astashahada, stashahada au ujuzi wa vitendo, huku wakiaminiwa na kutoa mchango katika maeneo mbalimbali.

Kwa vijana wenye kiu ya kupata shahada licha ya kupata matokeo ya chini, amesema bado wanaweza kutafuta fursa za kujiendeleza, ikiwemo kusoma katika baadhi ya vyuo vya nje ya nchi vinavyokubali sifa walizonazo au kuanza fani nyingine ili kujenga sifa zinazohitajika.

Aidha, Dkt. Ngosha amewashauri vijana kuangalia pia mafunzo ya muda mfupi yenye mahitaji katika soko la ajira, hususani katika sekta ya afya.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni teknolojia ya tiba ya figo (Dialysis), Anesthesia, Ultrasound, Perfusion pamoja na Critical Care na Trauma Management.

Amesema wataalamu wenye ujuzi katika maeneo hayo wana nafasi ya kutoa huduma muhimu katika sekta ya afya kutokana na uhitaji wa wataalamu wa vitendo.

Aidha, ameitaka jamii kubadili mtazamo unaotafsiri shahada kuwa kipimo pekee cha elimu na mafanikio, badala yake kuzingatia pia ujuzi wa vitendo na mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Amesema hatua hiyo inaweza kuwasaidia vijana kutumia fursa zilizopo na kujenga taaluma hata pale ambapo hawakufikia sifa za kujiunga moja kwa moja na shahada.