Mkuu wa wilaya ya Longido Salum Kalli akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla. Afisa mawasiliano kutoka shirika la GAIN ,Aileen Tinka akizungumza katika maadhimisho hayo.jijini Arusha leo

Happy Lazaro, Arusha.

Serikali imewataka wazazi, walezi, walimu na wanafunzi kujenga utamaduni wa unywaji wa maziwa nyumbani na shuleni, ikisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha lishe, afya na ustawi wa watoto pamoja na kujenga taifa lenye nguvu.

Hayo yamesemwa Septemba 30,2026 jijini Arusha na Mkuu wa wilaya ya Longido Salum Kalli kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha katika maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Duniani Kitaifa yaliyofanyika katika.viwanja vya Ngarenaro jijini Arusha .

Salum amesema kuwa kaulimbiu inayohamasisha unywaji wa maziwa nyumbani na shuleni inapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku na si jambo linalofanyika wakati wa maadhimisho pekee.

Amesema maziwa ni miongoni mwa vyakula vyenye virutubisho muhimu vinavyosaidia ukuaji wa mtoto, hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata maziwa mara kwa mara ili kujenga afya na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika masomo na shughuli nyingine za kijamii.

Amesema kuwa ,uwekezaji katika lishe ya mtoto ni uwekezaji katika Taifa la sasa na lijalo, kwa kuwa mtoto mwenye afya bora ana nafasi kubwa ya kukua vizuri, kujifunza kwa ufanisi na baadaye kuwa mzalishaji na mshiriki muhimu katika maendeleo ya Taifa.

“Serikali inaendelea kuimarisha mpango wa unywaji wa maziwa shuleni ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya mpango huo yanahitaji ushirikiano wa wazazi, walimu, maafisa lishe, wataalamu wa mifugo, halmashauri, wafugaji, wasindikaji na sekta binafsi.”amesema Salum.

Aidha, amesema matumizi ya maziwa yana faida zaidi ya lishe kwa kuwa yanaimarisha mnyororo wa thamani wa sekta hiyo, ambapo ongezeko la mahitaji huleta fursa kwa wafugaji, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na wawekezaji katika viwanda na teknolojia.

Ametoa wito kwa wafugaji kuongeza uzalishaji wa maziwa yenye ubora kwa kuzingatia ufugaji wa kisasa, lishe bora ya mifugo, afya na ustawi wa wanyama pamoja na usafi wakati wa kukamua na kuhifadhi maziwa.

Aidha ameitaka sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika uzalishaji, ukusanyaji, uchakataji, ufungashaji, usafirishaji na usambazaji wa maziwa ili kuongeza thamani ya bidhaa hiyo na kuhakikisha maziwa bora na salama yanawafikia walaji wengi zaidi.

Amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwahamasisha watoto kutumia fedha wanazopewa kununua vyakula vyenye manufaa kwa afya, ikiwemo maziwa na bidhaa zake kama mtindi, badala ya kutumia fedha hizo kwenye vinywaji na bidhaa zisizokuwa na mchango mkubwa katika lishe.

Salum amewataka wanafunzi kutambua kuwa afya ni mtaji wao wa kufanya vizuri katika masomo na maisha ya baadaye, akisisitiza kuwa lishe bora humsaidia mtoto kukua vizuri, kuwa na afya njema na kuwa na uwezo wa kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Ameongeza kuwa , mtoto anayejengewa msingi mzuri wa lishe leo ndiye atakayekuwa daktari, mwalimu, mfugaji, mwanasheria, mwandishi, mjasiriamali, mwanasayansi, kiongozi au mzalishaji wa taifa hapo baadaye, hivyo kila hatua ya kuboresha lishe ni uwekezaji kwa kizazi kijacho.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kushirikiana na wadau kuimarisha mazingira ya uzalishaji na ukusanyaji wa maziwa, miundombinu, uchakataji na upatikanaji wa maziwa yenye ubora na usalama.

Mtaalamu wa lishe mradi wa mageuzi ya Tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi(C-SDTP) Dkt . Mackrina Mombo aliyemwakilisha Mratibu wa mradi amesema kuwa , mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini kwa kuhimiza ufugaji wenye tija na unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, huku pia ukitoa elimu ya lishe kwa wanafunzi na kuhamasisha unywaji wa maziwa.

Mombo amesema kwa mwaka huu mpango wa unywaji wa maziwa shuleni utatekelezwa katika shule 18 Tanzania Bara na Visiwani, huku jamii ikihimizwa kuchagua maziwa badala ya vinywaji visivyo na virutubisho.

Kwa upande wake Afisa mawasiliano kutoka shirika la GAIN ,Aileen Tinka amesema GAIN ni shirika la kimataifa linalofanya kazi kuhakikisha jamii zinapata lishe bora na kupunguza utapiamlo, hususani kwa watoto. ambapo GAIN inaunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha mpango wa lishe na ulaji shuleni.

 “Kwa sasa, GAIN inashirikiana na Galaxy Food & Beverages na Arla Foods katika sekta ya maziwa, kuhakikisha wanafunzi wanapata yoghurt zilizoongezwa virutubishi.”amesema Aileen . 

“Mradi huu unafadhiliwa na Austrian Development Agency (ADA) na unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro, ukilenga kufikia shule 120.”amesema