Mwalimu Mkuu wa Shule ya awali na msingi ya Miale, Obadia Mollel akizungumza kwenye mahafali hayo.jijini Arusha


Wahitimu wa darasa la saba katika shule ya awali na.msingi ya Miale wakiwa katika picha ya pamoja katika.mahafali hayo .
……….
Na Happy Lazaro, Arusha
WAHITIMU wa elimu ya msingi nchini wametakiwa kuwa makini wanapoingia katika mazingira mapya baada ya kumaliza elimu ya msingi, huku wakisisitizwa kuepuka makundi yasiyofaa yanayoweza kuwashawishi kujiingiza katika tabia zinazoweza kuathiri maisha na masomo yao ya baadaye.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mwalimu Mkuu wa Shule ya awali na msingi ya Miale, Obadia Mollel, wakati wa mahafali ya tisa ya Darasa la Saba, ambapo jumla ya wanafunzi 31 wamehitimu elimu yao ya msingi.
Mollel amesema baada ya kumaliza elimu ya msingi, wanafunzi watakutana na watu wenye tabia na mienendo tofauti, hivyo wanapaswa kuwa makini katika kuchagua marafiki na makundi ya kujiunga nayo ili waweze kulinda ndoto zao na kufikia malengo waliyojiwekea.
“Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, mtakutana na watu wenye tabia na mienendo tofauti, ni muhimu kuwa makini na kuchagua marafiki wanaoweza kuwajenga na kuwasaidia kufikia ndoto zenu,” amesema Mollel.
Aidha, amewataka wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao licha ya majukumu mbalimbali ya kutafuta maisha, akisisitiza kuwa mawasiliano ya karibu yanaweza kuwasaidia wazazi kugundua changamoto zinazowakabili watoto na kuwapatia ushauri kwa wakati.
Amesema wazazi wanapaswa kujenga uhusiano wa karibu na watoto wao kwa kuishi nao kama marafiki, hali itakayowafanya watoto kuwa huru kueleza mambo yanayowasumbua na kupata mwongozo unaofaa, hasa wanapoanza safari mpya ya elimu na maisha baada ya kumaliza elimu ya msingi.
Katika upande wa taaluma, Mollel amesema kiwango cha ufaulu katika shule hiyo kimeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka kutokana na juhudi za walimu, wanafunzi na wazazi katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.
Mollel amesema wanafunzi hao tayari wamefanya Mtihani wa Taifa wa Kumaliza Elimu ya Msingi na shule ina matumaini makubwa ya kuona wakipata matokeo bora zaidi kutokana na msingi walioupata shuleni hapo, huku wastani wa ufaulu ukiwa katika daraja A.
Naye mgenirasmi katika mahafali hayo Katibu wa wilaya ya Arumeru ,Valentine Joseph amewataka wahitimu hao kuongeza bidii zaidi katika.masomo yao kwani wanaenda hatua nyingine ambayo inahitaji umakini wa hali juu .
“Kumaliza darasa la.saba ndo mwanzo wa elimu napenda mtambue kuwa ndo safari inaanza nawasihi muongeze bidii katika masomo yenu huku mkiepuka makundi yasiyofaa kwani yatawaharibia malengo yenu mliyojiwekea.”amesema Valentine.
