Dar es Salaam, Septemba 29, 2026. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 18,078.41 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika katika mikoa 14 nchini kati ya Julai na Septemba 2026.

Kamishna Mkuu wa DCEA, Kamishna Aretas Lyimo, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu operesheni zilizofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Amesema kati ya kiasi hicho, kilogramu 11,504.76 zilikuwa bangi, kilogramu 6,529.5 mirungi, kilogramu 44.45 bangi aina ya skanka na gramu 41.25 heroin. Katika operesheni hizo, watuhumiwa 289 walikamatwa, ambapo 169 wamefikishwa mahakamani na taratibu za kisheria zinaendelea dhidi ya wengine.

Kwa mujibu wa Kamishna Lyimo, operesheni hizo pia ziliwezesha kukamatwa kwa magari nane, bajaji moja na pikipiki 40 zilizotumika katika shughuli zinazohusiana na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Amesema bangi imeendelea kuongoza kwa kiwango cha uzalishaji na ukamataji, hususan katika mikoa ya Morogoro na Tabora. Morogoro, kilogramu 6,299.24 za bangi pamoja na kilogramu 226 za mbegu za bangi zilikamatwa, huku Tabora kilogramu 4,650.86 za bangi pamoja na kilogramu 203 za mbegu za bangi zikikamatwa.

Kuhusu mirungi, Kamishna Lyimo amesema operesheni zimebaini matumizi ya pikipiki na mabasi ya abiria katika usafirishaji wa dawa hiyo, hususan katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma, ambapo jumla ya kilogramu 6,412.89 za mirungi zilikamatwa.

Amesema katika moja ya matukio hayo, watuhumiwa watatu walikamatwa wakisafirisha bunda 238 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 125.33 kwa kutumia basi la kampuni ya RATCO lenye namba za usajili T.443 EMG, lililokuwa likifanya safari kati ya Tanga na Dar es Salaam.

Aidha, amesema mkoani Tabora, Wilaya ya Uyui, kilogramu 21.95 za bangi zilikamatwa katika gari aina ya TATA lenye namba za usajili T.381 DWU, lililokuwa likifanya safari kati ya Uyui na Kahama, huku watuhumiwa watano wakikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Kutokana na hali hiyo, Kamishna Lyimo amewataka wamiliki na waendeshaji wa mabasi na magari ya abiria kuimarisha udhibiti wa mizigo, ukaguzi wa vyombo vya usafiri pamoja na usimamizi wa wafanyakazi ili kuzuia vyombo vyao kutumika katika usafirishaji wa dawa za kulevya.

Amesema katika eneo la ukaguzi wa abiria katika Bandari ya Dar es Salaam, DCEA ilibaini matukio ya usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia abiria, ambapo raia wa Uturuki alikamatwa akiwa na gramu 1.87 za bangi aina ya skanka, raia wa Kenya akiwa na gramu 3.89 za mirungi na raia wa Nigeria akiwa na gramu 4.6 za bangi. Aidha, mkoani Arusha, raia wawili wa Afrika Kusini walikamatwa wakiwa na jumla ya gramu 65.8 za bangi aina ya skanka.

Katika operesheni hizo, DCEA pia ilizuia kuingia nchini kwa shehena ya sulphuric acid yenye uzito wa kilogramu milioni 64 baada ya kubaini kupitia mfumo wa kielektroniki kuwa taarifa zilizowasilishwa kuhusu uingizaji wa kemikali hiyo hazikuwa sahihi na matumizi yake halali hayakuwa yamebainishwa. Aidha, pikipiki zimeendelea kutumika katika usafirishaji wa mirungi, hasa katika ukanda wa kaskazini wa Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

Kamishna Lyimo amesema pamoja na mafanikio hayo, Mamlaka imebaini kuwepo kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu walio nje ya DCEA wanaodaiwa kutumia mwanya wa udhibiti wa biashara ya dawa za kulevya kujihusisha na vitendo vya rushwa na uhalifu. Amesema baadhi yao wamekuwa wakiwalenga wahalifu wa biashara hiyo, kuwakamata na kuwanyang’anya dawa hizo kisha kuwashinikiza kutoa rushwa, huku wengine wakiwatishia kuwafikisha kwenye Mamlaka endapo watakataa kutekeleza matakwa yao, hivyo amewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na dawa za kulevya ili hatua za kisheria zichukuliwe.