Mwamvua Mwinyi, Pwani
Septemba 28, 2026
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini, Mwalimu Mwajuma Nyamka, ameiomba Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kushughulikia maeneo hatarishi likiwemo eneo la Mwanalugali, kabla ya mvua zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwezi Oktoba mwaka huu.
Nyamka amesema maeneo hayo yakiwemo Mwanalugali na Muheza yana historia ya kujaa maji wakati wa mvua kubwa, hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na makaravati madogo yasiyoweza kupitisha maji mengi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maandalizi ya CCM katika kuunga mkono na kusimamia utekelezaji wa tahadhari dhidi ya mvua hizo, Nyamka amesema tayari chama hicho kimekutana na viongozi mbalimbali, wenyeviti wa serikali za mitaa pamoja na mabalozi, kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari.
Amesema TARURA imekuwa ikielezwa mara kwa mara kuhusu changamoto hizo na tayari imechukua hatua katika baadhi ya maeneo, lakini Mwanalugali bado inahitaji kushughulikiwa kwa haraka, hasa kutokana na utabiri wa mvua za El Niño.
Nyamka amesema katika eneo la Mwanalugali, karavati lililowekwa halipo kwenye mkondo wa asili wa maji, hivyo maji yanaponyesha hufuata mkondo wake na kulifanya karavati hilo kutokuwa na ufanisi wa kutosha.
Ameiomba TARURA kutumia hata fedha za dharura kushughulikia changamoto hiyo ili kuzuia madhara kwa wananchi, akisema hata mvua za kawaida zimekuwa zikileta changamoto katika eneo hilo.
Nyamka pia amewataka wananchi kuzingatia usafi wa mazingira kwa kutotupa taka ovyo, huku akizitaka serikali za mitaa kuweka na kusimamia sheria ndogo za kudhibiti uchafuzi wa mazingira ili kuepusha magonjwa ya mlipuko.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuwaelimisha watoto kuepuka kucheza kwenye mashimo, madimbwi na maeneo yenye maji wakati wa mvua, kwa kuwa yanaweza kuhatarisha usalama wao.
