NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Isimani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda, ametoa jezi kwa timu tatu zilizoshika nafasi ya kwanza hadi ya tatu katika mashindano ya Mgongolwa Super Cup 2026 yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kata ya Kihorogota Wilaya ya Iringa Vijijini.
Jezi hizo zilikabidhiwa kwa timu Bingwa Kihorogota fc, Mshindi wa Pili Ivangwa Fc na Mshindi wa Tatu Ndolela fc ikiwa ni sehemu ya zawadi na motisha kwa vijana waliojitokeza kushiriki mashindano hayo, yaliyolenga kukuza vipaji na kuhamasisha vijana kushiriki michezo.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge huyo, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini, Anold Mvamba, alimsifu Emanuela kwa kuwa mbunge anayetekeleza ahadi na kuendelea kuwaunga mkono vijana katika shughuli za michezo.
Mvamba alisema mchango wa mbunge huyo umeonyesha umuhimu wa viongozi kushirikiana na wananchi katika kuendeleza vipaji na kuimarisha michezo katika maeneo yao.
“Kiongozi anajulikana kwa mambo mawili; jambo la kwanza ni kutoa ahadi, lakini jambo la pili ambalo ni muhimu zaidi ni kutekeleza ahadi,” alisema Mvamba.
Alisema michezo si burudani pekee bali pia ni sehemu muhimu ya afya na maendeleo ya vijana, hivyo akawataka wananchi kuendelea kuunga mkono shughuli za michezo katika maeneo yao.
Mvamba pia alisema viongozi wa Wilaya ya Iringa Vijijini wataendelea kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Isimani pamoja na viongozi wengine kuhakikisha vijana wanapata fursa zaidi za kushiriki michezo na kuendeleza vipaji vyao.
Mashindano hayo ya Mgongolwa Super Cup 2026 yalishirikisha timu nane na yalifikia tamati katika Kata ya Ismani, huku viongozi wakimpongeza Diwani wa Kata hiyo, Michael Mgongolwa, kwa kuanzisha mashindano hayo kwa lengo la kukuza vipaji na kuhamasisha vijana kushiriki michezo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kihorogota Michael Mgongolwa, alisema mashindano hayo yalianza kwa kushirikisha timu nane na yalilenga zaidi kuibua vipaji vya vijana pamoja na kuongeza hamasa ya michezo katika kata hiyo.
Mgongolwa alisema katika mashindano hayo timu zilizofanikiwa kufika hatua ya mwisho zilipambana kutafuta mshindi wa kwanza, wa pili na wa tatu, huku zawadi zikitolewa kwa washindi kama sehemu ya kuhamasisha vijana kuendelea kushiriki michezo.
Alisema mshindi wa kwanza alitarajiwa kukabidhiwa ng’ombe mmoja mwenye thamani ya Sh800,000 na jezi, mshindi wa pili mbuzi wawili na jezi na mshindi wa tatu mbuzi mmoja pamoja na jezi.
Mgongolwa alisema wazo la kuanzisha mashindano hayo lilitokana na yeye, kabla ya kumshirikisha Mbunge wa Jimbo la Isimani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda, ambaye alikubali kushirikiana katika kuunga mkono mashindano hayo.
“Kwa kuhakikisha Kata ya Kihorogota inaendelea kung’ara, mashindano haya yameungwa mkono pia na Mbunge wetu wa Jimbo la Isimani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda,” alisema Mgongolwa.
Alisema baadhi ya zawadi zilizotolewa katika mashindano hayo zilipatikana kutokana na mchango wa mbunge huyo, ambaye aliendelea kuunga mkono juhudi za vijana katika michezo.
Awali, Mratibu wa Mashindano ya Mgongolwa Super Cup, Elieza Dononda, alisema mashindano hayo yalishirikisha timu nane tangu yalipoanzishwa na yalikuwa na lengo la kutoa nafasi kwa vijana kuonyesha vipaji vyao.
Dononda alisema timu hizo zilishindana hadi hatua za mwisho, huku timu mbili zikifika katika mchezo wa fainali, ambao uliwakutanisha Ivangwa fc na Kihorogota fc
Alisema mashindano hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano na Diwani wa Kata ya Ismani, Michael Mgongolwa, ambaye alianzisha mpango huo kwa ajili ya kuwaunganisha vijana kupitia michezo.
Hafla ya kufunga mashindano hayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na mamia ya wananchi, huku zawadi zikiwemo jezi zikikabidhiwa kwa timu zilizofanya vizuri katika Mgongolwa Super Cup 2026.

