NA DENIS MLOWE, IRINGA

WANACHAMA na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa wametakiwa kuendelea kuheshimu maadili ya chama na kujipanga kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya CCM, huku wakianza maandalizi ya mikakati ya kukiimarisha chama kwa miaka ijayo. 

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM, Idara ya Oganaizesheni, Paul Matiko Chacha, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Mkoa wa Iringa uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha UVCCM Ihemi.

Chacha alisema CCM ilianzishwa Februari 5, 1977, ikiwa na lengo kuu la kushika dola, hivyo chama kinapoelekea kutimiza miaka 50 ni muhimu viongozi na wanachama kutumia kipindi hicho kutafakari safari ya chama, mafanikio yaliyopatikana na mipango ya kukiendeleza katika miaka ijayo.

Alisema maandalizi hayo yanapaswa kuanzia sasa ili kuhakikisha chama kinaweka mikakati madhubuti ya muda mrefu kuelekea kutimiza miaka 100.

Kwa upande wake, Mjumbe wa NEC CCM, Salim Abri ‘Asas’, aliwataka viongozi wa CCM Mkoa wa Iringa kutumia maadhimisho ya miaka 50 kufanya tathmini ya hali ya chama na kuweka mikakati mipya ya kukiimarisha.

Alisema viongozi waliopo sasa wanapaswa kuhakikisha wanaacha alama katika chama, akieleza kuwa kizazi kijacho kitauliza viongozi waliokuwepo wakati wa maadhimisho hayo walifanya nini katika kukijenga chama.

Asas pia alisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya chama, ikiwemo ofisi za CCM katika ngazi za kata na mazingira ya watumishi wa chama nakuwataka viongozi na wanachama kujiandaa vizuri kuelekea uchaguzi, huku akisisitiza umuhimu wa mchakato wa uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu na wanachama kuendelea kushirikiana katika kukijenga na kukiimarisha chama.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, alisema ushirikiano uliopo kati ya CCM na Serikali umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa, akieleza kuwa viongozi wa chama wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kusimamia utekelezaji wa shughuli na miradi mbalimbali. 

Alisema mkoa unaendelea kutekeleza Ilani ya CCM chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Yassin alisema Serikali imeendelea kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Iringa, jambo alilosema limewezesha kuonekana kwa miradi katika maeneo mbalimbali. 

Alisema hakuna wilaya isiyokuwa na miradi ya maendeleo, huku akieleza kuwa chama kinajivunia juhudi za Serikali katika kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa na wananchi wanaendelea kunufaika na miradi hiyo.

Yassin aliwataka wajumbe wa mkutano huo kutoka wakiwa na ari ya kutekeleza maelekezo na maazimio yatakayotolewa na kumshukuru Asas kwa mchango wake katika kukisaidia chama, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano, umoja na kauli moja miongoni mwa wanachama wa CCM Mkoa wa Iringa katika kuendeleza chama na maendeleo ya mkoa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema hali ya uzalishaji, uchumi na uwajibikaji wa wananchi mkoani humo imeendelea kuimarika, sambamba na ushirikiano mzuri kati ya CCM na Serikali.

James alisema Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya uzalishaji na uchumi, ikiwemo kuboresha miundombinu inayosaidia shughuli za kiuchumi na imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wanafunzi na kuboresha mazingira ya walimu kwa kujenga ofisi na nyumba za walimu pamoja na kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi ili sekta hiyo iendelee kuwa na ufanisi.

Alisema madiwani wa CCM wameendelea kuiwakilisha chama katika mabaraza ya madiwani kwa kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Ilani katika ngazi za halmashauri. Aidha, alisema wabunge wa CCM na madiwani katika mkoa huo wameendelea kutekeleza wajibu wao wa kushirikiana na wananchi na Serikali katika kufuatilia utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo.

James alisema viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali wameendelea kutumia mikutano yao kuwaelimisha wananchi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo changamoto za mvua. 

Alisema hali ya utekelezaji wa miradi, ukusanyaji wa mapato na ushirikiano kati ya wananchi na Serikali imeendelea kuwa nzuri.