Na Silivia Amandius. Pwani.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo, amewapongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kurahisisha mfumo wa utoaji wa risiti za kielektroniki, akisema hatua hiyo inasaidia kupunguza gharama kwa walipakodi na kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiari.

Kanali Kolombo ameyasema hayo leo Septemba 25, 2026, alipolitembelea banda la TRA katika maonesho ya Mafia Festival 2026 yanayofanyika katika viwanja vya Utende, Wilaya ya Mafia, mkoani Pwani. Amesema mfumo wa IDRAS umewezesha kurahisishwa kwa utoaji wa risiti, hivyo kuwataka wananchi wote kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi sahihi ya risiti za kielektroniki.

“Mfumo wa kutoa risiti sasa umerahisishwa zaidi, hivyo utachochea ulipaji kodi wa hiari na sote tuwe mabalozi wa kuhamasisha matumizi sahihi ya risiti za kielektroniki,” amesema Kanali Kolombo.

Kwa upande wake, Afisa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Bi. Yusta Kaunda, amesema mamlaka hiyo inashiriki maonesho ya Mafia Festival 2026 kwa kutoa huduma na elimu mbalimbali za kodi. Huduma hizo ni pamoja na upatikanaji wa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN), uwasilishaji wa ritani za kodi, masuala ya forodha, leseni za udereva, matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD/VFD), stempu za kielektroniki za kodi (ETS), pamoja na elimu ya kodi katika sekta ya utalii na uwekezaji na matumizi ya mfumo wa IDRAS.

Aidha, Bi. Yusta amewakumbusha wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi ya mapato kwa awamu ya tatu kabla au ifikapo Septemba 30, 2026, ili kutimiza wajibu wao wa kikodi kwa wakati.