Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wataalamu wa afya ya macho duniani wamewahimiza wazazi nchini Tanzania kuhakikisha watoto wao wanapimwa macho kabla ya shule kufunguliwa kwa muhula mpya, wakisema hatua hiyo inaweza kuwa na mchango mkubwa katika elimu na maisha yao ya baadaye.
Ushauri huo unatokana na takwimu za Shirika la Kimataifa la Kuzuia Kupotea kwa Uwezo wa Kuona (IAPB), zinazoonyesha kuwa upimaji rahisi na wa kawaida wa macho pamoja na matumizi ya miwani unaweza kusaidia kuongeza maradufu mapato maishani ya mtoto anayekulia Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sababu kuu ya watoto kutokuona vizuri inatokana na matatizo ya macho yasiyosahihishwa, hali inayoweza kuathiri uwezo wa mtoto kuona vizuri na kujifunza darasani.
IAPB inaeleza kuwa tatizo hilo husababisha watoto nchini Tanzania kupoteza jumla ya miaka 27,178 ya masomo shuleni, kutokana na changamoto za kuona ambazo zinaweza kutambuliwa na kusahihishwa.
Hata hivyo, iwapo tatizo la kuona litatambuliwa mapema mtoto akiwa na umri wa miaka mitano na kusahihishwa kwa matumizi ya miwani bora hadi atakapofikisha miaka 18, mapato yake ya maisha yanaweza kuongezeka kwa asilimia 124.
Takwimu hizo ni sehemu ya matokeo mapya ya utafiti wa IAPB unaoonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 23 ambako usahihishaji wa matatizo ya kuona unaweza kuongeza maradufu mapato ya maisha ya mtoto.
Kwa msingi huo, IAPB imewahimiza wazazi wenye watoto wadogo kuhakikisha wanawapeleka kupima macho mara kwa mara, huku ikisisitiza umuhimu wa watoto kuanza au kurejea shuleni wakiwa na uwezo mzuri wa kuona.
Aidha, IAPB imezindua kampeni ya “Yapende Macho Yako Shule Zinapofunguliwa” (Love Your Eyes Back-to-School), inayolenga kuongeza uelewa kuhusu afya ya macho ya watoto kupitia maelezo yanayotolewa shuleni, darasani na nyaraka fupi zinazoweza kupelekwa kwa wazazi na walezi.
Afisa Mkuu Msimamizi wa IAPB, Peter Holland, amesema upimaji rahisi na wa kawaida wa macho pamoja na miwani unaweza kuwa miongoni mwa uwekezaji muhimu zaidi ambao mzazi anaweza kufanya kwa ajili ya maisha ya baadaye ya mtoto.
Holland amesema baadhi ya wazazi wanaweza kushindwa kupanga au kugharamia huduma za upimaji wa macho na miwani, hivyo amezitaka serikali kuhakikisha kila mtoto anapata huduma hizo na anapata fursa ya kuona vizuri anapoingia shuleni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kifundi wa Afya Shirikishi katika Sightsavers, Sumrana Yasmin, amesema kila mtoto anastahili kupata nafasi ya kuona, kujifunza na kushamiri, akisisitiza kuwa uwekezaji katika afya ya macho unaweza kusaidia kuzuia upotevu wa uwezo wa kuona na kuwapa watoto nafasi ya kutumia uwezo wao kikamilifu.
Naye Mkurugenzi wa Miradi wa CharityVision International, Anadine Marshall, amesema mtoto ambaye hawezi kuona ubao darasani anaweza kuchukuliwa kimakosa kuwa hajifunzi, wakati upimaji rahisi wa macho unaweza kubaini tatizo na kusaidia kuliondoa kwa kumpatia mtoto miwani inapohitajika.
Wito huo umetolewa kuelekea Mkutano wa Ulimwengu wa Wakuu wa Nchi kuhusu Afya ya Macho unaotarajiwa kufanyika Antigua na Barbuda Novemba 2, ambapo wakuu wa nchi na washirika wanatarajiwa kuweka ahadi za kuimarisha afya ya macho duniani.
