Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeadhimisha Siku ya Usalama wa Mgonjwa kwa kutoa elimu kwa wagonjwa kuhusu haki zao na kuwakumbusha watumishi kuhusu wajibu wa kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma salama na bora.
Akizungumza Septemba 24, 2026 katika kilele cha maadhimisho hayo yaliyofanyika hospitalini hapo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt. Abdalah Baja, amesema maadhimisho hayo yamejikita katika mambo mawili, ikiwemo kutoa elimu kwa wagonjwa kuhusu haki zao pamoja na kuwajengea uwezo watumishi kuhusu utoaji wa huduma unaozingatia usalama wa wagonjwa.
Dkt. Baja amesema wagonjwa wana haki ya kupata huduma kwa viwango vinavyokubalika na gharama halisi, kulindwa usalama wao, kuhudumiwa kwa wakati na kupata huduma zinazozingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa ya ubora wa huduma za afya.
Ameongeza kuwa wagonjwa pia wana haki ya kupata huduma bila kupendelea, kuheshimiwa na kuheshimu mawazo yao, kupata ushauri na elimu kuhusu huduma zinazotolewa BMH, pamoja na kupewa taarifa sahihi kwa umma kwa lugha nyepesi na kujengewa uhusiano mzuri na watoa huduma.
Ametaja haki nyingine ni kufuatiliwa kwa maendeleo ya wagonjwa waliolazwa baada ya kutoka hospitalini, kushirikishwa katika kuboresha huduma za hospitali, pamoja na kupokelewa, kusikilizwa na kushughulikiwa kwa malalamiko yao huku wakipewa mrejesho.
Amesema ushirikishwaji wa wagonjwa ni muhimu katika kuboresha huduma kwa kuwa maoni yao yanaisaidia hospitali kufahamu namna wanavyozipokea huduma na maeneo yanayohitaji maboresho ili kufikia lengo la kutoa huduma bora na salama zaidi.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa BMH, Dkt. Kakorongo Mugisha, amesema hospitali hiyo imekuwa ikiadhimisha Siku ya Usalama wa Mgonjwa tangu mwaka 2023 kwa kuwajengea uwezo wagonjwa na kuboresha mifumo ya utoaji huduma, huku akisisitiza kuwa BMH inahakikisha usalama wa mgonjwa tangu anapofika hospitalini hadi anapoondoka. Amesema huduma za dharura zinapatikana saa 24 kwa siku, siku saba za wiki na siku 365 kwa mwaka.
Baadhi ya wagonjwa waliopata huduma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wameeleza kuridhishwa na huduma wanazopata, huku wakitaja usafi wa mazingira, upatikanaji wa huduma na ushirikishwaji wa wagonjwa katika matibabu kuwa miongoni mwa mambo wanayoyathamini.
Joyna Nyembela, ambaye amesema amekuwa akipata matibabu BMH tangu Januari 2025 kutokana na changamoto ya magoti yote mawili, amesema alifanyiwa upasuaji wa goti la kwanza Mei 2025 na la pili Juni 2026, na anaendelea vizuri huku akiwapongeza madaktari kwa huduma wanazotoa.
Lilian Wambura, aliyefika hospitalini hapo kumsindikiza ndugu yake kwa matibabu, amesema ameridhishwa na usafi wa mazingira na huduma zinazotolewa.
Naye, Jasery Zacharia, mkazi wa Shinyanga, amesema amefanyiwa upasuaji mara mbili kutokana na tatizo la mawe kwenye figo na amekuwa akishirikishwa katika maamuzi kuhusu matibabu yake, akieleza kuwa amepata huduma nzurikutoka kwa madaktari.

( PICHA NA FULLSHANGWE BLOG )
