Na Hellen Mtereko, Mwanza

Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza imekabidhi magari matatu aina ya Toyota Probox yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 80 kwa Jeshi la Polisi Mkoani humo, kwa ajili ya kuimarisha doria katika barabara kuu na kukabiliana na ajali za barabarani.

​Akikabidhi magari hayo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza leo, Septemba 23, 2026, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Fabian Chacha, amesema ununuzi wa magari hayo ni muendelezo wa juhudi za kuongeza nguvu katika doria.

Amessema kuwa awali kamati hiyo ilikabidhi magari matatu na makabidhiano ya leo ya magari mengine matatu yanafanya jumla ya magari yaliyokabidhiwa kufikia sita.

​Akipokea na kuyazindua magari hayo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amewashukuru wadau hao kwa msaada huo unaolenga kuongeza nguvu katika doria za barabarani.

Aidha, ameahidi kuyatunza na kuyatumia ipasavyo ili kudhibiti ajali zinazosababisha watu kupoteza maisha pamoja na uharibifu wa miundombinu.

​Akifafanua jinsi magari hayo yatakavyotumika, Kamanda Mutafungwa amesema tayari wameshayagawanya kwa wakuu wa upelelezi na usalama barabarani katika wilaya za Misungwi, Magu na Sengerema.

​”Gari la kwanza litakwenda Wilaya ya Magu kwa ajili ya doria katika barabara kuu; gari la pili litakwenda Wilaya ya Sengerema kuhudumia kwenye barabara kuu inayotoka Mwanza kwenda Mikoa ya Geita na Kagera na gari la tatu litakwenda Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya doria katika barabara kuu inayotoka Mwanza kwenda Mkoa wa Shinyanga,” amefafanua Kamanda Mutafungwa.

​Kamanda Mutafungwa amemtaka Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza SSP Sunday Ibrahim na wasaidizi wake kuhakikisha wanayatumia magari hayo kufanya doria za kuwakamata madereva wote wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani kwa lengo la kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.