Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Mashariki kwa kushirikiana na DCEA na MSD, imetoa mafunzo kwa Waganga Wafawidhi, Wafamasia na Wauguzi kutoka Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze, juu ya utunzaji na uhifadhi wa dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mganga Mkuu wa Bagamoyo, Dkt. Ubwe Yasin, ameipongeza TMDA na kusema mafunzo hayo ni muhimu kwani halmashauri yake ina vituo viwili vya waraibu na kama dawa hizo hazitatunzwa vizuri zinaweza kutumika kama vilevi na kuathiri jamii.

Mwakilishi wa DCEA, Mfamasia Upendo Chenya, amesema wameshuhudia ongezeko la matumizi holela ya dawa kama Pethidine, Morphine, Diazepam (Valium) na Tramadol, hivyo kuna haja ya udhibiti mkali na dawa hizo zitolewe kwa cheti cha daktari pekee, huku waraibu wakielekezwa kwenye vituo vya MAT.

Mkaguzi Mkuu wa Dawa TMDA Kanda ya Mashariki, Dkt. Bahati Yakobo, amewataka watoa huduma kuimarisha ulinzi wa dawa hizo na kuzingatia utunzaji sahihi ili zisiingie kwenye matumizi yasiyo kusudiwa, kwani matumizi holela husababisha utegemezi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bagamoyo, Dkt. Lyana Lymo, ameishukuru TMDA na kuahidi kusambaza elimu hiyo kwa wenzake ili kuhakikisha matumizi sahihi na ulinzi wa dawa hizo.

Mfamasia wa Bagamoyo TC, Mohammed Said Rwaub, amesema mafunzo hayo yatakuwa chachu kwao katika kufuata sheria kwani Serikali inatumia fedha nyingi kuhudumia waraibu.

Mwakilishi wa MSD, Suzana Majule, amesema wataendelea kutoa elimu ya jinsi ya kuomba na kuhifadhi dawa hizo na usambazaji wake lazima uambatane na kibali kutoka TMDA.