Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imezindua mashindano bab kubwa ya mchezo wa mpira wa miguu yatakayojulikana Kama _Rhino Cup_ kutoa hamasa kwa jamii ya tarafa ya Ngorongoro yenye vijiji 25 na Kata 11 kutoshana nguvu katika mchezo wa kabumbu.
Mashindano hayo yamefunguliwa jumanne hii katika viwanja vya shule ya msingi Makao Ngorongoro na kocha wa zamani wa timu ya taifa (Taifa Stars ) na Yanga Charles Boniface Mkwasa.
Akifungua mashindano hayo Mkwasa amewataka vijana wa tarafa ya Ngorongoro kutumia michezo Kama fursa ya ajira na kujenga afya zilizo bora na kuhimiza uhifadhi shirikishi kupitia michezo.
Naibu kamishna wa Uhifadhi NCAA Aidan Makalla amesema Mamlaka imeamua kuanzisha kombe hilo litakalochezwa kila mwaka ili kutoa hamasa ya mchezo wa mpira wa miguu ndani ya tarafa ya Ngorongoro na kuhamasisha jamii juu ya ulinzi wa faru na rasilimali mbalimbali zilizopo ndani ya hifadhi.
Mashindano hayo yatashirikisha kata 11 za tarafa ya Ngorongoro na bingwa wa mashindano hayo pamoja na zawadi nyingine ataenda kushuhudia mtanange wa ligi kuu baina ya Simba na Yanga kwa msimu wa mwaka huu.

