NA DENIS MLOWE, IRINGA

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa,. Nancy Nyalusi, amewawezesha wanawake wa Kata ya Ulanda, Jimbo la Kalenga, Wilaya ya Iringa, kwa kutoa Shilingi milioni tatu kwa ajili ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi kupitia majukwaa na vikundi vya wanawake.

Nyalusi ametoa fedha hizo wakati wa ziara yake katika Kata ya Ulanda, ambapo alikutana na wanawake na kusikiliza changamoto pamoja na mahitaji mbalimbali yanayowakabili katika shughuli zao za kiuchumi.

Akizungumza katika ziara hiyo, Nancy Nyalusi amesema uwezeshaji huo ni sehemu ya jitihada za kuwaunga mkono wanawake ili waweze kuimarisha shughuli zao za uzalishaji, kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia zao.

Amesema wanawake wana nafasi kubwa katika maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuwawezesha kwa kuwapatia mitaji na fursa zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.

“Nawaomba mtumie fedha hizi kwa malengo yaliyokusudiwa. Zitumieni katika shughuli zitakazozalisha kipato, kuimarisha vikundi vyenu na kuhakikisha wanachama wengine pia wananufaika,” amesema Nyalusi.

Aidha, amewataka wanawake hao kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao na kuhakikisha uwezeshaji wanaoupata unakuwa chachu ya kukuza shughuli zao za ujasiriamali badala ya kutumika kwa matumizi yasiyokuwa na tija.

Nyalusi amesema kuwa kupitia vikundi na majukwaa ya wanawake, wananchi wanaweza kujenga nguvu ya pamoja katika kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na biashara na shughuli nyingine za uzalishaji.

Wanawake wa Kata ya Ulanda wamepokea uwezeshaji huo huku wakisisitizwa kuwa na usimamizi mzuri wa fedha hizo ili ziweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa na kunufaisha wanachama kwa muda mrefu.