Na Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog,Dodoma 

TAASISI na kampuni zitakazochelewesha taarifa zinazohitajika katika Uhamasishaji, Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), au kutoa taarifa za uongo, zimenywa kuwa zinaweza kukutana na mkono wa Sheria na kutozwa faini hadi Sh milioni 100 kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa TEITI, Balozi Wilson Masilingi, ametoa onyo hilo alipozungumza na waandishi wa Habari Septemba 22, 2026, jijini Dodoma, ambapo amesema baadhi ya taasisi zinasuasua kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwa ajili ya uhakiki wa mapato yanayotokana na rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia.Balozi Masilingi, amesema TEITI ina mamlaka ya kisheria ya kuchukua hatua dhidi ya taasisi au kampuni zinazokiuka matakwa ya Sheria ya TEITI ambayo katika vifungu vya 23 na 24 vya sheria hiyo, taasisi au kampuni itakayowasilisha taarifa za uongo, kuchelewesha taarifa au kuzuia wataalamu wa TEITI kupata taarifa, inaweza kutozwa kiasi hicho.Amebainisha kuwa TEITI, hadi sasa haijaanza kutumia mamlaka hayo dhidi ya wanaochelewesha taarifa, akisema hatua hiyo imekuwa ikizingatiwa kutokana na ushirikiano uliopo kati ya taasisi hiyo na wadau wake.

Pia, ameseme Kuwa TEITI imepewa muda na Bunge kukamilisha uhakiki wa taarifa hizo na kuandaa taarifa itakayowasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana ya Madini kwa ajili ya kupelekwa Bungeni.

Ametaja baadhi ya Taasisi ambazo TEITI inahakiki taarifa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), NEMC, Ofisi ya Msajili wa Hazina, mifuko ya hifadhi ya jamii, PURA, OSHA na Wakala wa Vipimo Tanzania.

Amesema uhakiki huo unalenga kujiridhisha kuhusu mapato yanayotokana na rasilimali hizo, ikiwemo fedha zinazowasilishwa Serikalini pamoja na fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika jamii.

Balozi Masilingi amewataka wananchi kutoa taarifa kwa TEITI kuhusu hoja zinazohusu matumizi ya fedha zinazotokana na michango ya kampuni za madini na gesi asilia kupitia utaratibu wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ili ziweze kuhakikiwa kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Kwa upande mwingine ameomba ushirikiano wa vyombo vya habari akisema ni muhimu katika kufuatilia mapato na matumizi ya fedha zinazotokana na rasilimali za wananchi, pamoja na kuwafahamisha wananchi kuhusu kazi zinazofanywa na TEITI.