Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 katika mji wa Korogwe, Tanga amepewa siku tisa kuhakikisha ameanza majaribio ya kuyatoa maji kutoka kwenye kidakio na kuyapeleka katika mtambo wa kutibu maji e ( WTP) ili ifikapo Novemba 2026 maji yafike kwa wananchi.
Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso (Mb) amemtaka mkandarasi kutekeleza hayo wakati akikagua maendeleo ya mradi wa maji wa Miji 28 katika mji wa Korogwe leo Septemba 21, 2026.
“Mkandarasi nakupa siku tisa tu kuanzia leo Septemba 21, Hadi ifikapo Septemba 30 uwe umeshaanza majaribio kutoa maji mtoni na kuyapeleka eneo la kutibu” Mhe Aweso amesema.
Pamoja na hilo amewataka wataalamu wa Wizara ya Maji kukaa mguu sawa kuhakikisha mwaka 2026 – 2027 unatekelezwa mpango wa kufikisha maji katika vijiji 400 kwasababu serikali imeshatenga fedha kwa kazi hiyo.
Waziri Aweso amezitaka mamlaka za maji nchini pamoja na bodi za maji za mabonde kufanya tathmini ya miundombinu ya mabomba ili kubaini mabomba ambayo yanaweza kuathiriwa na mvua za El-nino na kufanya ukarabati kabla hayajaleta shida kwa wananchi mvua zitakapoanza.
Mradi wa Maji wa Miji 28 Korogwe unatazamiwa kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi mapema mwezi Desemba 2026 ukinufaisha wilaya nne za Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani.

