Mwamvua Mwinyi, Pwani

Septemba 21, 2026

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amewataka Wakuu wa Wilaya zote mkoani humo kushirikiana na wadau kupitia Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa na kuwasilisha maoni yatakayosaidia kuboresha maudhui yake.

Amesema ushirikishwaji huo utasaidia kuwa na mwongozo wenye taarifa sahihi, unaoendana na mahitaji ya sasa na unaoweza kuitangaza Pwani kama eneo lenye fursa mbalimbali za uwekezaji.

Nyongo ametoa agizo hilo Septemba 21, 2026, wakati akiongoza kikao cha wadau wa uwekezaji kilichofanyika Kibaha kwa ajili ya kupitia na kuhuisha Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa.

Amesema mwongozo huo uliotolewa mwaka 2019 umefikia wakati wa kuhuishwa kutokana na mabadiliko yaliyotokea katika kipindi cha miaka sita, ikiwemo kuongezeka kwa fursa za uwekezaji, miundombinu na shughuli za uzalishaji.

“Tumeamua kuhuisha muongozo huu kwa sababu mambo mengi yamebadilika, Tumepokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau ambayo yatasaidia kufanya maboresho na kuandaa muongozo unaoendana na mahitaji ya sasa,” amesema.

Nyongo amesisitiza kuwa Pwani ni Mkoa wa viwanda na wenye umuhimu wa kimkakati katika uchumi wa Taifa, hivyo Mwongozo huo mpya unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu ya kutangaza fursa za uwekezaji na kuwawezesha wawekezaji kufanya maamuzi sahihi.