Na Farida Said Morogoro

Serikali imeitaka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kuipa kipaumbele tafiti za kubaini viashiria vya moto wa misitu mapema na kuboresha usimamizi wa moto katika maeneo ya hifadhi, ili kulinda misitu, bioanuai na shughuli za utalii.

Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Hamad Hassan Chande ametoa agizo Septemba 21, 2026, wakati akizindua Bodi ya 13 ya Wakurugenzi ya TAFORI kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na utalii Dkt. Ashatu Kijaji ambapo amesema tafiti zinapaswa kutoa majibu ya kisayansi kuhusu moto unaotumika kama sehemu ya usimamizi wa maeneo ya hifadhi, pamoja na njia za kuzuia moto usio wa lazima na kutoa tahadhari mapema.

Pia ameielekeza TAFORI kuongeza uwezo wa maabara za ndani kupima usalama na ubora wa asali, akisema Tanzania inalenga kutumia fursa ya masoko ya nje, ikiwamo Ulaya, bila kulazimika kupeleka sampuli nje ya nchi. Amesema uwezo huo utapunguza gharama za vipimo na kuongeza ushindani wa asali ya Tanzania.

Aidha ameitaka Bodi kusimamia Mpango Mkakati wa TAFORI wa miaka mitano, 2026/27–2030/31, unaolenga kuimarisha tafiti na matumizi ya matokeo yake katika uhifadhi na maendeleo ya sekta.

Amesema katika kipindi cha Bodi ya 12, TAFORI ilikamilisha tafiti 17, zikiwamo saba za kimkakati, zilizohusu maeneo kama umri wa uvunaji wa misindano na misaji, Alama ya Asali ya Tanzania (Honey Trademark), mchango wa misitu na nyuki katika pato la Taifa kupitia Green Accounting, pamoja na changamoto za ufugaji nyuki. Serikali pia imewezesha fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Makao Makuu, ujenzi wa Kituo cha Utafiti Tabora, uboreshaji wa maabara na ununuzi wa vitendea kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, amesema taasisi hiyo itatekeleza maelekezo ya Wizara na kuendelea kuimarisha tafiti zenye tija kwa uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na nyuki. Amesema TAFORI pia itaendelea kujenga uwezo wa watafiti kupitia mafunzo ya juu na uzoefu ndani na nje ya nchi, huku ikiimarisha ushirikiano na taasisi za kitaifa na kimataifa katika tafiti za misitu na ufugaji nyuki.