Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Septemba 20, 2026

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Pwani yaanza utekelezaji agizo la kukagua miundombinu ya barabara na madaraja hatarishi na kurekebisha ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa.

Aidha imebaini jumla ya maeneo 221 yenye hatari ya mafuriko, ambapo 138 yako katika kiwango cha juu cha uhatarishi na 83 yakiwa katika kiwango cha kati.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Ibrahim Kibasa, amesema wakala huo unaendelea kufanya tathmini ya maeneo hayo kwa kushirikisha wataalamu, huku hatua za awali zikichukuliwa ikiwemo kusafisha mifereji, makaravati na njia za kupitisha maji ili kupunguza athari kwa wananchi na miundombinu ya barabara.

Amesema kazi za tathmini na udhibiti wa mtiririko wa maji zinaendelea katika maeneo ya Chumbi, Muhoro na Ikwiriri wilayani Rufiji, huku maeneo mengine yakiendelea kufanyiwa uchambuzi kulingana na kiwango cha hatari kilichobainika.

Kibasa amesema TARURA pia inatumia vikundi maalumu vya kufanya usafi wa mifereji, makaravati na kuzibua maeneo yanayoweza kuzuia mtiririko wa maji, ambapo kwa sasa vikundi 23 vinafanya kazi wilayani Rufiji.

Amesema mpango huo ni kuendelea kuongeza vikundi hivyo katika halmashauri nyingine ikiwemo Kibaha, Kisarawe na Bagamoyo, huku maeneo yanayoendelea kufanyiwa tathmini yakijumuisha Delta ya Rufiji, Kibiti na Mkuranga.

“Tunaendelea kuainisha maeneo hatarishi ambayo yamekuwa yakiripotiwa na kutafuta njia mbadala za kukabiliana na changamoto hizo, pamoja na kutoa elimu ya usalama wa matumizi ya barabara katika maeneo hayo,” amesisitiza Kibasa.

Ameongeza kuwa TARURA itashirikiana na Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine kutoa tahadhari kuhusu matumizi salama ya barabara katika maeneo yenye hatari, huku timu za mwitikio wa dharura zikiwa zimeundwa katika ngazi ya Mkoa, Wilaya na TARURA Taifa.

Kwa mujibu wa Kibasa, timu hizo zitashirikiana na timu za maafa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, TANROADS, TANESCO, mamlaka za maji, Jeshi la Polisi, waandishi wa habari pamoja na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara katika kukabiliana na dharura endapo zitatokea.

Amesema TARURA Pwani tayari imejiandaa kwa vifaa vya dharura ikiwemo makaravati ya plastiki 30, vikapu 60 vya kuweka mawe pamoja na vifaa vingine vitakavyotumika katika maeneo yatakayokumbwa na changamoto.

Kwa upande wake, Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Kibaha, David Kakole, ameeleza wanaendelea na matengenezo ya miundombinu ya barabara, ikiwemo barabara ya kimkakati inayoelekea Kituo cha Reli ya Kisasa (SGR) Soga, pamoja na kurekebisha maeneo yenye changamoto ili kuboresha usafiri na kurahisisha shughuli za wananchi.

Naye Meneja wa TARURA Wilaya ya Bagamoyo, Bupe Angetile, amesema wanaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali, Wizara na Mkoa katika kujiandaa na tahadhari zinazohusiana na mvua za El Niño.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo amesema serikali imejipanga huku akisisitiza TARURA na TANROADS kukagua madaraja yote hatarishi na kuyarekebisha .

Ameeleza madaraja ambayo yanaendelea na hatua mbalimbali za ujenzi , wakandarasi wahakikishe wanakamilisha kazi kwa wakati.