Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, leo, Septemba 18, 2026, ametoa maagizo kwa uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhusu hatua za kuchukua ili kuongeza ufanisi na kuimarisha utendaji wa Wakala huo. 

Maagizo hayo yametolewa wakati wa kikao kati ya Msajili wa Hazina na uongozi wa TANROADS katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Dar es Salaam, huku ujumbe wa TANROADS ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Mha. Mohamed Besta.

Maagizo hayo yamelenga kuhakikisha TANROADS inaendelea kuimarisha ufanisi, uwajibikaji na tija katika utekelezaji wa majukumu yake, pamoja na kuongeza thamani ya uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya barabara.

OTR ina jukumu la kusimamia uwekezaji na maslahi ya Serikali katika taasisi na kampuni za umma, zikiwemo kampuni ambazo Serikali ina hisa chache. 

Kwa sasa, OTR inasimamia jumla ya taasisi na kampuni 308.