Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu baada ya Sala ya Ijumaa, alipofungua rasmi Ijitimai iliyoandaliwa na Jumuiya ya Tabligh Markaz Zanzibar, katika eneo la Bungi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, tarehe 18 Septemba, 2026.
…………
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza viongozi wa dini ya Kiislamu kuendelea kusisitiza umuhimu wa amani, upendo, umoja na mshikamano katika jamii, sambamba na kuimarisha malezi ya watoto na vijana katika misingi ya maadili mema.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 18 Septemba 2026, baada ya Sala ya Ijumaa, alipofungua rasmi Ijitimai iliyoandaliwa na Jumuiya ya Tabligh Markaz Zanzibar katika eneo la Bungi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema Masheikh na wahadhiri wanaoshiriki katika Ijitimai hiyo wana nafasi muhimu ya kuendelea kuwakumbusha waumini kuhusu mambo ya kheri, kuimarisha maadili na kujenga familia na jamii zinazozingatia mafundisho ya dini.
Rais Dkt. Mwinyi pia amewahimiza waumini na wananchi wanaoshiriki Ijitimai hiyo kuwa mabalozi wazuri wa mafundisho watakayoyapata, kwa kuyatafakari na kuyatekeleza katika maisha yao ya kila siku kwa manufaa yao, familia na jamii kwa ujumla.
Akizungumzia malezi ya vijana, Rais Dkt. Mwinyi amesema mabadiliko ya kijamii pamoja na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari yanaongeza umuhimu wa wazazi, walezi na viongozi wa dini kushiriki kwa karibu katika malezi ya watoto.
Amesema malezi bora yanapaswa kuanza mapema, huku wazazi na walezi wakiwa karibu na watoto wao na kuwajengea uwezo wa kutambua mema na mabaya katika mazingira yanayobadilika.
Alhaj Dkt. Mwinyi amesema mitandao ya kijamii ina fursa nyingi za manufaa, ikiwemo kupata elimu na mafundisho ya dini, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kufuatilia aina ya taarifa na maudhui yanayowafikia watoto na vijana kupitia majukwaa hayo.
Dkt. Mwinyi amewahimiza wananchi kuchukua tahadhari kutokana na taarifa za mamlaka husika kuhusu mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha, na kuzingatia maelekezo yatakayotolewa kwa ajili ya kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Amesisitiza umuhimu wa kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Taifa na majanga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, huku viongozi wa dini wakiendelea kusaidia katika kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuchukua tahadhari.
Akizungumzia amani na utulivu, Rais Dkt. Mwinyi amesema mazingira ya amani yaliyopo nchini imeendelea kutoa nafasi kwa shughuli mbalimbali za kidini, kijamii na kiuchumi kufanyika, pamoja na kuwezesha wageni kutoka maeneo na mataifa mbalimbali kutembelea Zanzibar.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kudumisha mazingira hayo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi na viongozi wa dini kuendelea kuwa sehemu ya kujenga maelewano na mshikamano katika jamii.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa Jumuiya katika kuimarisha miundombinu na huduma muhimu zitakazosaidia shughuli za kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.
Amesema Serikali inaendelea na mipango ya kuboresha barabara na miundombinu mingine, ikiwemo barabara kutoka Mjini kuelekea eneo hilo, ambayo imepangwa kuendelezwa kwa kiwango cha njia nne ili kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameeleza umuhimu wa kuendelea kuimarisha huduma katika eneo hilo, ikiwemo miundombinu ya elimu ya dini kama madrasa, ili kukidhi mahitaji ya jamii inayozunguka.
Ijitimai hiyo, iliyowakutanisha waumini kutoka mataifa mbalimbali duniani wenye lugha na tamaduni tofauti, imefunguliwa rasmi leo na itafanyika kwa muda wa siku tatu, huku washiriki wakipata mafundisho ya dini, kushiriki dua na shughuli mbalimbali zinazolenga kuimarisha umoja, mshikamano na maadili mema katika jamii.

