Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Baran Sillo (wa pili kutoka kulia), akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mkutano wa Kwanza wa Wabunge Wanawake wa Kanda ya Maziwa Makuu, unaotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Novemba.

Katika picha ni pamoja na Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa sasa wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson; Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima; pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Bw. Adam Mihayo.

…………… 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametangazwa kuwa Mgeni Rasmi wa Mkutano wa Wanawake Wabunge 2026 (WPC), unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 2 hadi 5 mwaka huu, ukiwakutanisha wanawake wabunge kutoka nchi 12 wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR).

Tangazo hilo limetolewa leo Septemba 18, 2026, wakati wa hafla ya kifungua kinywa kwa viongozi waandamizi na wanahabari iliyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, ambapo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa ICGLR (FP-ICGLR) walizindua rasmi maandalizi ya mkutano huo wenye kaulimbiu, “Kwa Ukanda wa Maziwa Makuu Wenye Amani na Maendeleo.”

Mbali na Rais Samia, Mkutano huo unatarajiwa kumshirikisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Judith Suminwa Tuluka, akiwa mgeni maalumu wa ngazi ya juu, huku Spika wa Mabunge, taasisi za kikanda, mashirika ya Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia, mitandao ya wanawake, vijana na washirika wa maendeleo wakishiriki.

Akitoa tangazo hilo, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Baran Sillo, amesema Tanzania inatumia nafasi ya kuwa mwenyeji kuendeleza historia yake katika juhudi za kujenga amani, usalama, umoja na ushirikiano katika Ukanda wa Maziwa Makuu, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na michakato ya kufanya maamuzi.

Sillo amesema mkutano huo utatoa nafasi kwa wanawake wabunge kubadilishana uzoefu na kuimarisha mitandao ya ushirikiano baina ya mabunge, sambamba na kujadili mikakati ya vitendo ya kukabiliana na changamoto za amani, usalama na maendeleo zinazolikabili eneo hilo.

Kwa mujibu wa FP-ICGLR, moja ya maeneo muhimu yatakayojadiliwa ni kuimarisha nafasi ya wanawake katika kuzuia migogoro, upatanishi na ujenzi wa amani, huku wanawake wabunge wakitumia nafasi zao katika utungaji wa sheria na michakato ya kibunge kusaidia kujenga jamii zenye amani na usalama.
Mkutano huo pia utajadili matumizi ya nyenzo za kibunge na kisheria katika kuendeleza usalama, utulivu na utawala jumuishi, ikiwemo kuongeza ushiriki wa wanawake katika upangaji wa bajeti, usimamizi na ufuatiliaji wa utendaji wa Serikali pamoja na michakato ya kufanya maamuzi.

Eneo jingine la kimkakati litakuwa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kijamii, ambapo sekta binafsi na wadau wengine wanatarajiwa kushirikishwa katika kutafuta njia za kuongeza fursa za wanawake katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo yanayozingatia usawa wa kijinsia.

Akizungumzia ajenda hiyo, Katibu Mkuu wa FP-ICGLR, Balozi Dkt. Deo Mwapinga, amesema ushiriki wa wanawake wabunge unatarajiwa kuongeza sauti za wanawake katika mifumo ya kidemokrasia kupitia uwakilishi, utungaji wa sheria, usimamizi wa Serikali na diplomasia ya kibunge.

Mkutano huo utaendeleza pia ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama iliyoainishwa katika Azimio Namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huku Tanzania ikishirikisha uzoefu wake kupitia Mpango Kazi wa Taifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2025/2026.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Tanzania itatumia mkutano huo kushirikishana uzoefu katika kuimarisha usawa wa kijinsia na uwakilishi wa wanawake na wanaume, akisisitiza kuwa historia ya wanawake katika ujenzi wa taifa, amani na diplomasia ni sehemu muhimu ya mjadala huo.

Mkutano huo pia utalenga kuimarisha ushirikiano kati ya mabunge, asasi za kiraia, taasisi za kikanda na washirika wa kimataifa, ili kuhakikisha mapendekezo yatakayojadiliwa yanahusisha mitazamo ya wadau mbalimbali na kutafsiriwa katika hatua zinazotekelezeka.

FP-ICGLR imesema miongoni mwa matokeo yanayotarajiwa ni kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam kuhusu wanawake, amani, usalama na maendeleo, pamoja na mpango kazi utakaoweka hatua za utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa katika mkutano huo.

Mkutano wa Wanawake Wabunge 2026 unatokana na uamuzi wa Mkutano wa 15 wa Kawaida wa Baraza Kuu la FP-ICGLR uliofanyika Luanda, Angola, Aprili 2025, kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake wabunge katika uongozi na michakato ya kufanya maamuzi katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.