CPA. Daniel Warungu, Mkurugenzi Mtendaji wa TOL PLC (kushoto), akiwa pamoja na Bw. Leonard Kitoka, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TOL PLC (kulia), wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano uliofanyika katika ofisi za TOL PLC, Dar es Salaam, kuhusu uzinduzi wa Toleo la Haki Stahiki (Rights Issue) lenye lengo la kukusanya shilingi bilioni 8.17 kutoka kwa wanahisa wa kampuni hiyo. Fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa kituo kipya cha uzalishaji wa gesi ya Carbon Dioxide (CO₂).
………..
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TOL Gases PLC imezindua rasmi Toleo la Hisa za Haki Stahiki (Rights Issue) lenye thamani ya Shilingi bilioni 8.17, likiwa na lengo la kuongeza uwezo wa uzalishaji wa hewa ya Carbondioxide (CO2) na kukidhi ongezeko la mahitaji ya gesi za viwandani na tiba nchini Tanzania na katika masoko ya kikanda.
Kupitia toleo hilo, kampuni inatoa hisa mpya za kawaida 11,501,193 kwa bei ya Shilingi 710 kwa kila hisa, huku wanahisa waliopo wenye sifa wakistahili kupata hisa mpya moja kwa kila hisa tano za kawaida walizokuwa nazo hadi Tarehe ya Kumbukumbu ya Septemba 14, 2026.
Toleo hilo limefunguliwa Septemba 17, 2026 na litafungwa Oktoba 8, 2026 saa 10:00 alasiri, huku hisa mpya zikitarajiwa kuorodheshwa na kuanza kuuzwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) Oktoba 22, 2026 kwa kuzingatia masharti ya uorodheshaji.
Fedha zitakazopatikana zitatumika hasa katika ujenzi wa kiwanda kipya cha uzalishaji wa CO2, ikiwemo usanifu, ununuzi, ufungaji na uanzishaji wa kiwanda hicho pamoja na mahitaji ya kiuendeshaji na kilogistiki yatakayohusiana na mradi huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TOL Gases, CPA Leonard Kitoka, amesema uzinduzi wa Toleo la Hisa za Haki unaashiria hatua ya kampuni kutoka kipindi cha kujiimarisha kibiashara kuelekea awamu mpya ya uwekezaji na kuongeza uwezo wa uzalishaji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita TOL imeimarisha biashara, uendeshaji na uwezo wake wa uzalishaji na usafirishaji, huku mapato yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 9.5 kwa mwaka kati ya 2020 na 2025, na EBITDA kuongezeka kwa asilimia 28 kati ya mwaka 2024 na 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases, Bw. Daniel Warungu, amesema uwekezaji huo unalenga kushughulikia changamoto ya uwezo wa uzalishaji ambao kwa sasa umeanza kuzidiwa na ongezeko la mahitaji ya bidhaa za kampuni, hali inayopunguza uwezo wa TOL kuhudumia kikamilifu baadhi ya fursa za ndani na kikanda.
Warungu amesema kampuni inaendelea na mpango mpana wa kuongeza uwezo wa uzalishaji, ambapo pia inajiandaa kuanzisha Kitengo kipya cha Kutenganisha Hewa chenye uwezo wa tani 13 kwa siku, ambacho kikijumuishwa na kitengo kilichopo cha tani saba kwa siku, kinatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa oxygen na nitrogen hadi takribani tani 20 kwa siku ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026.
Aidha, TOL inaongeza magari ya usambazaji na kujenga vituo vipya vya usambazaji vya kikanda katika mikoa ya Arusha na Mtwara, sambamba na kituo kilichopo Mwanza, hatua inayolenga kusogeza huduma na uhakika wa usambazaji karibu zaidi na wateja nchini Tanzania na katika masoko ya kikanda.
Upanuzi huo ni sehemu ya mkakati wa ukuaji wa TOL wa mwaka 2025 hadi 2029, unaolenga kujenga uwezo wa uzalishaji, kuimarisha uaminifu wa huduma na kuiwezesha kampuni kutumia fursa zinazotokana na kuongezeka kwa mahitaji ya gesi za viwandani na tiba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TOL Gases inahudumia sekta za afya, chakula na vinywaji, uchimbaji madini, uzalishaji viwandani na ujenzi, huku bidhaa zake zikijumuisha oksijeni, naitrojeni, hewa ya ukaa, asetilini, argoni, heliamu na gesi nyingine za viwandani na tiba.
Wanahisa wenye sifa wanaweza kuchukua sehemu yote au sehemu ya haki zao, huku watakaotumia haki zao zote wakiwa na fursa ya kuomba hisa ambazo hazitachukuliwa na wanahisa wengine, kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika Prospectus ya Toleo la Hisa za Haki. Tanzania Securities Limited (TSL) ndiyo Mshauri Mkuu wa Muamala na Wakala wa Udhamini, huku National Bank of Commerce Limited ikiwa Benki Mpokezi wa toleo hilo.

