Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange amesema TANESCO imejipanga vizuri kukabiliana na dharura zinazoweza kujitokeza katika kipindi cha mvua za El Nino ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya umeme kwa usalama. Bw. Twange ameyasema hayo katika Kipindi cha Aridhio kinachorushwa na TBC1 kuhusu hatua zinazochukuliwa na TANESCO katika kukabiliana na athari za Mvua za El Nino ziilizotabiriwa na mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA).
………..
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema limejipanga kukabiliana na athari za mvua za El Niño kwa kuimarisha miundombinu, kuandaa timu za dharura na kuchukua tahadhari katika mabwawa ya kuzalisha umeme.
Akizungumza katika kipindi cha Aridhio cha TBC, Septemba 17, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema shirika limefanya tathmini ya miundombinu yake na kubaini maeneo hatarishi.
“Tumefanya kikao na Mamlaka ya Hali ya Hewa na tathmini ya miundombinu yetu, hivyo maeneo hatarishi tunayafahamu na tumeanza kuchukua hatua,” amesema Bw. Twange
Amesema maandalizi hayo yameanza pia katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, kwa kuimarisha nguzo za umeme zilizoonekana kuwa katika hali ya kuchoka.
“Kama Dar es Salaam tumeanza, kwa ajili ya kurekebisha nguzo za miti ambazo zina dalili ya kuchoka ili tuweze kuweka nguzo nyingine,” ameongeza Bw. Twange.
Aidha, amesema TANESCO imeandaa timu za dharura zitakazoshughulikia changamoto za wateja endapo zitatokea wakati wa mvua hizo.
“Tumeziandaa timu zetu za dharura kwa maana ya _“emergency”_ team zetu kwa maana ya kushughulika wateja wetu watakapokuwa wanatupigia simu,” amethibitisha.
Kwa upande wa mabwawa ya kuzalisha umeme wa maji, amesema TANESCO inafuatilia hali ya maji katika mabwawa yake, huku ikitambua uwezekano wa El Niño kusababisha ongezeko kubwa la maji.
“Sisi tuna eneo jingine la vituo vyetu vya kuzalisha umeme wa maji. Mabwawa kama Mwalimu Nyerere, Mtera, Kidatu, Kihansi. Maji kwetu ni huduma muhimu na tunayafurahia kwa ajili ya kuwa na kiwango cha kutosha cha maji kinachotuwezesha kuzalisha umeme,” amesema.
Hata hivyo, amesema maji mengi kupita kawaida yanaweza pia kuwa na madhara kwa wananchi wanaoishi karibu na mabwawa hayo, hivyo TANESCO imeanza kutoa elimu na kuchukua tahadhari.
“Lakini kutokana na El Niño huenda tukapata maji mengi kuliko ilivyo kawaida. Na maji yale yanaweza kuleta madhara kwa majirani ambao wanazunguka maeneo ya mabwawa yetu,” ameongeza
“Tumeshaanza kazi kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo hayo kutoa elimu kwa wananchi lakini ni sisi wenyewe kuchukua tahadhari ili maji yatakapokuwa mengi basi yasije yakaleta madhara kwa majirani na wananchi walio karibu na mabwawa yetu ya kuzalisha umeme,” ameongeza Twange.
TANESCO imesema itaendelea kuchukua tahadhari na kuimarisha utayari wake kukabiliana na athari za El Niño, huku wananchi wakihimizwa kushirikiana na shirika hilo kwa kutoa taarifa mapema na kuzingatia usalama wa umeme.
