Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude akizungumza wakati akitembelea mabanda katika kliniki hiyo inayoendelea mkoani Arusha. 

…………

Happy Lazaro,Arusha.

Arusha , Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali na wafanyabiashara nchini, huku Kliniki ya Biashara na Viwanda inayoendelea jijiji Arusha ikitarajiwa kuwafikia zaidi ya wajasiriamali na wafanyabiashara 3,500 kutoka mikoa ya Kaskazini.

Akizungumza jijini Arusha wakati wa kufungua rasmi kliniki hiyo, Mkuu wa wilaya ya Arusha,Joseph Mkude amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera, mikakati na programu mbalimbali za Serikali zinazolenga kujenga uchumi shirikishi na kuongeza fursa za wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Amesema kliniki hiyo inatoa huduma mbalimbali ikiwemo usajili wa majina ya biashara, utoaji wa leseni za biashara za kundi A na B, elimu kuhusu ubora, vipimo na viwango, taarifa za masoko na mwenendo wa bei, pamoja na elimu kuhusu teknolojia rahisi za uzalishaji.

“zaidi ya Taasisi 20 zinazohusika na huduma za biashara, viwanda na uwekezaji zimeshiriki katika kliniki hiyo, zikitolea wananchi huduma na elimu kuhusu kodi, bima, masoko, uzalishaji unaozingatia viwango, matumizi ya nembo ya “Made in Tanzania” pamoja na fursa za mikopo yenye masharti nafuu.”amesema Mkude .

Amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kurasimisha biashara zao ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo huduma za kifedha, masoko na ushauri wa kitaalamu, akiwataka wajasiriamali wa Arusha kutumia fursa hizo kikamilifu.

Aidha, amesema Arusha ina fursa kubwa za biashara na uwekezaji katika sekta za utalii, kilimo, mifugo na uzalishaji, huku akibainisha kuwa maandalizi kuelekea kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON yanaweza kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara.

Kwa upande wake Mratibu wa kliniki ya viwanda na biashara inayoendelea mkoani Arusha ,Milton Manyara amesema kuwa ,

Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendesha kliniki hiyo jukwaa linalozikutanisha taasisi wezeshi katika sekta ya biashara na viwanda ili kutoa huduma mbalimbali kwa wafanyabiashara na wajasiriamali katika eneo moja.

Manyara amesema kuwa ,kupitia kliniki hiyo, wafanyabiashara wanapata huduma na elimu kuhusu usimamizi wa biashara, viwango na ubora wa bidhaa, mikopo pamoja na fursa mbalimbali za uwezeshaji zinazotolewa kupitia programu zilizo chini ya SIDO.

Amesema kuwa,wananchi wanapatiwa elimu kuhusu namna ya kufikia masoko ya ndani na nje kwa kuzingatia viwango, ubora na mahitaji ya masoko, hususan fursa zinazotokana na soko la pamoja la Afrika na maandalizi ya mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika katika ukanda huu.

“Business Clinic imeanzishwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wafanyabiashara kwa kuwakutanisha watoa huduma mbalimbali katika eneo moja, badala ya mfanyabiashara kulazimika kufuata ofisi moja baada ya nyingine.”amesema Manyara.

Aidha amewataka Wafanyabiashara na wajasiriamali wa Jiji la Arusha kutumia fursa hiyo kujifunza, kusajili na kurasimisha biashara zao ili zitambulike na ziweze kunufaika na huduma pamoja na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.

Kliniki hiyo ilianza Septemba 14 na inatarajiwa kufungwa Septemba 19 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Ngarenaro, ambapo wananchi wa Arusha na maeneo jirani wametakiwa kujitokeza kupata huduma na elimu kuhusu namna ya kufanya biashara katika mfumo rasmi.