Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawataarifu wananchi na umma kwa ujumla kuwa, limefanikiwa kumkamata Emmanuel Elisante Mariki (28), Mkulima na mkazi wa Kijiji cha Lyamungo, Kata ya Marangu, Wilaya ya Moshi, ambaye alikuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujeruhi watu wawili katika tukio lililotokea tarehe 24 Agosti, 2026.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa kumi na nusu alfajiri, katika Kijiji cha Lyamungo, Kata ya Marangu Mashariki, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwashambulia na kuwajeruhi watu wawili, ambao ni Scola Bernad (23), pamoja na mtoto wa mama huyo aitwaye Kelvin Baraka (02), kwa kutumia kitu chenye ncha kali.
Katika tukio hilo, mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwashambulia na kuwakata sehemu mbalimbali za miili yao, huku Scola Bernad akijeruhiwa vibaya na kutenganishwa viganja vya mikono yake, kabla ya mtuhumiwa huyo kutokomea kusikojulikana baada ya kutenda tukio hilo.
Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro lilianza msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na wananchi na hatimaye kufanikiwa kumkamata tarehe 13 Septemba, 2026, majira ya saa sita mchana, katika eneo la Bonite Shirimatunda, Wilaya ya Moshi, alikokuwa amejificha.
Mtuhumiwa huyo anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya taratibu za uchunguzi na hatua nyingine za kisheria na baada ya taratibu hizo kukamilika, atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashukuru wananchi wote waliotoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zilizowezesha kupatikana na kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
Jeshi la Polisi linaendelea kuwasisitiza wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi hilo kuhusu watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
