Na Abdallah Nassoro – MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeanza kutumia teknolojia ya kisasa kutoa matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa ubongo kwa wagonjwa wa kiharusi inayoongeza ufanisi wa matibabu hayo.

Mkurugenzi wa Upasuaji wa Ubongo MOI, Dkt. Lemeri Mchome amesema leo Septemba 17, 2026 kuwa teknolojia hiyo ni ya kwanza kutumika nchini na kwamba italeta mapinduzi katika matibabu ya kiharusi.

“Tunatoboa tundu dogo kichwani na kupitisha kifaa maalum chenye kamera ambacho kinaenda kutonyesha eneo ambalo damu imevilia na kutuwezesha kuitoa bila kuathiri sehemu nyingine”, amesema Dkt. Lemeri.

“Hii ndiyo teknolojia ya kisasa zaidi duniani na sisi kama taasisi hatuko nyuma, wagonjwa wa kiharusi hawana sababu ya kukimbilia nje ya nchi kwa matibabu, huduma hiyo inapatikana MOI. Kwa sasa tunapokea wagonjwa watatu hadi watano kwa siku, teknolojia hii imekuwa msaada wa matibabu bora”, ameongeza.

Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo MOI, Dkt. John Mtei ambaye ameshiriki katika upasuaji wa kwanza kwa kutumia kifaa hicho amesema, teknolojia hiyo inaacha alama katika mapinduzi ya tiba ya kiharusi nchini.

“Ufanisi wa matibabu ndiyo nyenzo muhimu katika matumizi ya teknolojia hii, mgonjwa anafanyiwa upasuaji na kuondolewa tatizo lake kwa uhakika”, amesema Dkt. Mtei.

Taasisi ya MOI imeendelea kujikita katika kuleta afua mbalimbali hapa nchini za kuipunguzia Serikali mzigo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa rufaa za gharama kubwa na pia kuendelea kuwa kituo cha weledi cha matibabu ya mifupa na mfumo wa fahamu barani Afrika.