Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji, Vodacom Business, Joseph Sayi, akizungumza na wafanyabiashara wa rejareja wa bidhaa za Tanzania Breweries PLC (TBL) wakati wa semina ya kuwajengea uwezo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (GRIT), iliyofanyika jijini Mwanza jana. Mafunzo hayo yaliyowashirikisha wafanyabiashara 150 yalilenga kuwaongezea ujuzi katika usimamizi wa biashara, fedha na matumizi ya suluhisho za kidijitali. Semina hiyo ni sehemu ya ushirikiano wa miaka miwili kati ya TBL na Vodacom Tanzania unaolenga kuwafikia zaidi ya wafanyabiashara 24,000 nchini.
………….
Zaidi ya wafanyabiashara 150 jijini Mwanza leo wamefanya mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo ili kuwasaidia kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi, kusimamia fedha na kuongeza faida, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (GRIT) unaotekelezwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa ushirikiano na Vodacom Tanzania Plc yamewaleta pamoja wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza kwa ajili ya kujifunza namna ya kuboresha usimamizi wa biashara, ikiwemo kupanga matumizi ya fedha, kudhibiti bidhaa na kufanya maamuzi yanayoweza kusaidia biashara zao kukua.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, alisema kuwa GRIT ni sehemu ya juhudi za kampuni hizo ili kuwawezesha wafanyabiashara wanaofanya kazi nazo kwa kuwapatia maarifa na ujuzi unaoweza kuwasaidia kusimamia biashara zao kwa ufanisi zaidi. Alisema uwezo wa kusimamia fedha, bidhaa na shughuli za kila siku ni muhimu katika kuweka biashara katika nafasi nzuri ya kukua na kuchangia maendeleo ya jamii.
Miongoni mwa wakufunzi katika mafunzo hayo ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dkt. Patrokil Kanje, aliyewafundisha washiriki namna ya kuendesha biashara kwa ufanisi, kusimamia gharama na kutambua maeneo yanayoweza kusaidia kuongeza faida.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Dkt. Kanje aliwasisitiza wafanyabiashara kuwa na uelewa wa kina kuhusu biashara zao, hasa katika kufuatilia mauzo, gharama na faida. Alieleza kuwa mfanyabiashara anapaswa kufahamu si tu kiasi anachouza, bali pia gharama anazotumia na faida anayobaki nayo, kwa kuwa taarifa hizo ni muhimu katika kufanya maamuzi sahihi, kudhibiti matumizi na kupanga ukuaji wa biashara.
Kwa mfanyabiashara, changamoto ya kila siku si kuuza bidhaa pekee. Ni kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika kwa uangalifu, bidhaa zinaendelea kuwepo, gharama zinasimamiwa na biashara inabaki na faida. Hivyo, mafunzo hayo yanaweka mkazo kwenye maarifa ambayo mfanyabiashara anaweza kuyatumia moja kwa moja katika biashara yake.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania Plc Joseph Sayi, amewahimiza wafanyabiashara kutumia suluhisho za kidijitali katika shughuli zao za kila siku, akieleza kuwa teknolojia inaweza kurahisisha miamala, kusaidia usimamizi wa fedha na kuimarisha mawasiliano na wateja.
Sayi alisema matumizi sahihi ya suluhisho za kidijitali yanaweza kuwasaidia wafanyabiashara kurahisisha baadhi ya shughuli za biashara, kupata huduma kwa urahisi na kutumia taarifa katika kufanya maamuzi yanayolenga kuimarisha biashara zao.
Mafunzo haya ni sehemu ya mpango wa miaka miwili kati ya TBL na Vodacom Tanzania unaolenga kuwafikia zaidi ya wafanyabiashara 24,000 wa TBL nchini.
Kupitia GRIT, wafanyabiashara wanatarajiwa kupata ujuzi katika maeneo mbalimbali muhimu kwa uendeshaji wa biashara, ikiwemo usimamizi wa mtaji na mtiririko wa fedha, udhibiti wa bidhaa, huduma kwa wateja, ukuaji wa biashara pamoja na matumizi ya teknolojia na suluhisho za kidijitali.
Kwa wafanyabiashara walioshiriki jijini Mwanza, mafunzo hayo yanatoa fursa ya kuangalia biashara zao kwa mtazamo mpana zaidi, si kwa kuzingatia mauzo ya siku hiyo pekee, bali namna ya kujenga biashara inayoweza kusimamiwa vizuri, kukabiliana na changamoto na kukua kwa muda mrefu.
Mpango huo unatarajiwa kuendelea kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini, ukiweka mkazo katika kuwapa maarifa na zana zinazoweza kuwasaidia kufanya biashara kwa ufanisi zaidi katika mazingira yanayozidi kubadilika.
